Saturday 24 October 2015

Hatimaye Wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Dodoma Waruhusiwa Kupiga Kura



MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Gallawa amesema wanafunzi wa vyuo vikuu waliojiandikisha Dodoma watapiga kura kwenye maeneo waliyojiandikisha.
 
Alisema hayo jana wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari juu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu utakaofanyika kesho.
 
Baadhi ya vyuo vya mkoa huo ni Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Chuo Kikuu cha St. John, Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Chuo cha Serikali za Mitaa, Chuo cha Mipango na Chuo cha Madini.
 
Akijibu moja ya maswali ya waandishi wa habari ni wapi wanafunzi wa vyuo vikuu watapiga kura kutokana na utata uliopo kuwa si wakazi wa mkoa wa Dodoma na kwamba kuna taarifa kuwa watasafirishwa kwa mabasi ili kufika Dodoma kupiga kura.
 
Gallawa alisema tume ilitaka watu wajiandikishe kituo chochote lakini kuna baadhi ya vituo viliandikisha watu wengi wa nje kuliko wakazi wa eneo husika, hali inayozua maswali mengi kuwa wakazi wa pale watachaguliwa diwani.
 
“Mfano utakuta kata ina watu 1,700 ambao si wakazi waliojiandikisha, wanafikia 5,000 lakini ukiangalia kwa undani suala hili utaona hali halisi ilivyo,” alisema.
 
Katika hatua nyingine, wasimamizi wa uchaguzi kwenye wilaya zote saba za mkoa wa Dodoma wameshapokea fedha za kuendesha uchaguzi mkuu na mafunzo kwa watendaji watakaoshiriki katika uchaguzi yanahitimishwa kwenye wilaya zote.
 
Waliojiandikisha ni wananchi 1,053,136 kuwa wapiga kura sawa na asilimia 102.7 ya lengo, ambapo lengo lilikuwa ni kuandikisha wapigakura 1,025,084.

0 comments: