Tuesday, 20 October 2015

Sababu Za Rais Kutovunja Baraza La Mawaziri Hadi Sasa Zawekwa Wazi



Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju ametoa mwongozo wa kisheria kufuatia sintofahamu iliyoibuka kwa baadhi ya watanzania kuhusu sababu zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kutovunjwa kwa baraza la mawaziri hadi muda huu huku zikiwa zimebaki siku tano kufanya uchaguzi mkuu.

Masaju alieleza kuwa kisheria bado sio muda muafaka wa kuvunja baraza la mawaziri kwa kuwa waziri hupoteza sifa za kuwa waziri wa serikali ya Tanzania punde kabla ya rais mpya kupatikana.

“Mara tu kabla rais mteule hajashika madaraka hayo, ndipo waziri anapoteza nafasi yake ya kuwa waziri. Kwahiyo sasa hata uchaguzi hatujafanya,” alisema.

Aliongeza kuwa suala la siku chache zilizobaki bado liko kisheria kwa kuwa rais mpya bado hajapatikana.

“Japokuwa ni siku tano sasa zimebaki, lakini uchaguzi ukishafanyika na rais akapatikana, mara tu huyu rais mteule hajashika madaraka hayo ndipo waziri anapoteza sifa ya kuwa waziri,” aliongeza.

Majibu ya kisheria ya mwanasheria mkuu wa serikali yamekuja wakati ambapo taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii na vijiweni zikieleza kuwa huenda kutovunjwa kwa baraza la mawaziri kunacheleweshwa kwakuwa kuna hofu ya mawaziri wengi kukihama Chama Cha Mapinduzi.

Balozi Juma Mwapachu alikoleza tetesi hizo wakati alipokuwa akirudisha kadi ya Chama Cha Mapinduzi katika ofisi za chama hicho zilizoko Mikocheni, Dar es Salaam baada ya kueleza kuwa uamuzi wake unaungwa mkono na mawaziri wengi wa serikali ya awamu ya nne.
 

0 comments: