Sunday, 25 October 2015

Vunjo: Wasimamizi Wawili wa Uchaguzi Wajeruhiwa Vibaya Baada Ya Kunaswa Wakisafirisha Kura FEKI


 

Wasimamizi wasaidizi watatu wamejeruhiwa kwa kipigo kutoka kwa wananchi waliowashuku kusafirisha masanduku yenye kura zilizokwishapigwa usiku wa kuamkia jana.

Tukio hilo liliwalazimu polisi kupiga mabomu ya machozi mfululizo kwa nyakati tofauti kati ya saa 5:00 na saa 8:00 usiku wa kuamkia jana ili kuwatawanya wananchi waliofurika kituo cha Polisi Himo.

Tafrani hiyo iliibuka baada ya wasimamizi hao wasaidizi kukamatwa na wananchi kati ya eneo la Marangu Kilema na mji mdogo wa Himo wakiwa na gari linalodaiwa ni la kada wa CCM.

Baada ya kukamatwa na masanduku hayo ya kura yakiwa na karatasi ambazo hazijapigwa bado, wananchi hao waliwatembezea mkong’oto wasimamizi hao na baadhi kujeruhiwa vibaya.

Kamanda wa Polisi mkoa Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani alisema kuwa wasimamizi hao walipigwa na wananchi baada ya kushukiwa kusafirisha masanduku ya kura ambayo yana kura zilizokwisha pigwa.

“Baada ya hao wasimamizi kukamatwa walipelekwa kituo cha Polisi Himo na taarifa zilizozagaa zilivuta wananchi wengi waliofurika kwenye hicho kituo,”alisema Kamanda Ngonyani.

Kamanda Ngonyani alisema polisi waliwataka wananchi hao kutawanyika lakini wakawa wanagoma na kuanzisha vurugu hali iliyowalazimu polisi kutumia nguvu ya ziada kuwatawanya.

Kituoni hapo alikuwepo pia mgombea Ubunge Jimbo la Vunjo kwa tiketi ya TLP, Agustino Mrema na hasimu wake mkubwa ambaye naye anagombea kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, James Mbatia.

Hata hivyo kamanda huyo alisema, baada ya kutokea kwa tafrani hiyo waliwasiliana na msimamizi wa uchaguzi, Fulgence Mponji ambaye baada ya kufika kituoni aliwatambua ni watumishi wa Tume.

Taarifa zaidi zinasema baada ya wasimamizi hao kufikishwa kituo cha polisi, wananchi walifunga barabara zote zinazoingia katika mji mdogo wa Himo huku wakikagua kila gari linalopita.

Madereva wa magari ambao walikaidi kusimama na kukaguliwa, walijikuta matatani kwa magari yao kuvunjwa vioo kwa kutumia mawe hali iliyowalazimu Polisi kutumia mabomu kuwatawanya.

Mrema alipotafutwa kuzungumzia hali hiyo, alisema asingeweza kusema chochote kuhusu uhalali wa karatasi hizo za kura kwani alimkabidhi jukumu hilo kijana wake ambaye alikuwa hajampata.
“Tukiwa pale polisi tuliambiwa kila mmoja ateue mtu atakayeshiriki kuzihakiki pamoja na msimamizi. Kuna kijana wangu nilimpa hiyo kazi mpaka sasa bado sijakutana naye anipe mrejesho,”alisema.

Kwa upande wake, Mbatia aliilaumu NEC kwa kutaka kuvuruga uchaguzi huo kwa kuwapa wasimamizi vifaa nyeti vya uchaguzi kuvisafirisha bila ulinzi wa Askari polisi au Mgambo.

0 comments: