Saturday, 3 August 2013

KODI YA SIMU IHAMISHIWE KENYE WAMILIKI WA NYUMMBA ZA KUPANGISHA

   NAIBU Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, amesema badala ya kuwatoza wananchi kwenye laini za simu serikali ihamishie kodi hiyo kwa wamiliki wa nyumba wanaopangisha bila kulipa kodi kwa Mamlaka ya Mapato (TRA).

Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, Makamba alisema kuwa malalamiko ya wananchi yalikuwa ya kweli na ya msingi hivyo basi serikali iweke mbadala wa tozo hizo kwa wenye nyumba za kupangisha.

Naibu waziri huyo aliongeza kuwa aliwahi kulizungumza hilo na kutoa ushauri kwa serikali na hata kuwasilisha hoja binafsi bungeni kuhusiana na suala hilo la kutaka wenye nyumba kulipa kodi ili ziweze 
kusaidia wananchi katika maeneo  mbalimbali ya maendeleo.

Alisema kodi kwenye tozo za simu wananchi walikuwa na hoja lakini aliwaita wabunge kuwa ni wanafiki kwa kuwa walipitisha wenyewe wakiwa kwenye kamati ya bajeti lakini akashangaa kuanza kulalama bila sababu kwa kile alichokiita ni kutaka sifa kwa wananchi.

“Kwa sasa tayari vikao vitatu vimefanyika lakini pia kuna haja ya kuangalia endapo hii itatolewa kutakuwa na mbadala gani wa kufidia hicho kiasi cha sh bilioni 178 kinachohitajika ili kuweza kutekeleza miradi mbalimbali ya wananchi vijijini,” alisema.

Hata hivyo alisema kuwa kikubwa ni kuganga yajayo na kuacha kukumbuka ya nyuma, kwamba wananchi wamelalamika na wamesikika na sasa maagizo aliyotoa rais wameanza kuyatekeleza.

Akijibu swali kuhusu kuongezeka kwa makato katika miamara ya kutuma na kupokea fedha kupitia simu za mikononi, Makamba alisema hana uhakika nalo, lakini ni wajibu wao kuliangalia upya suala hilo.

Source: Imeandikwa na Asha Bani, TanzaniaDaima

0 comments: