Saturday, 7 November 2015

Wastara Juma kuna uwezekano wa Kukatwa Mguu Tena


MASKINI wa Mungu! Baada ya kupata faraja kwa miaka kadhaa kwa kuwekewa mguu wa bandia, mwigizaji wa sinema za Kibongo, Wastara Juma, amepatwa na masaibu mengine ya kutakiwa kukatwa tena sehemu ya mguu uliokuwa umewekewa mguu wa bandia, Risasi Jumamosi lina stori nzima ya kusikitisha.

TATIZO LILIPOANZIA
Kwa mujibu wa ndugu wa karibu na Wastara ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini, tatizo linalosababisha mwigizaji kutakiwa kukatwa mguu huo wa kushoto lilimuanza alipokuwa kwenye kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) zilizomalizika Oktoba 24, mwaka huu.

“Tatizo lilimuanzia akiwa kwenye kampeni za CCM. Nafikiri kwenye mishemishe zile za kupanda majukwaani aliushtua, sasa ukawa unamuuma na yeye hakuweza kubaini mara moja tatizo ni nini. Kumbe mguu wake wa bandia pia ulikuwa umekatika vidole na kulika kwa chini ya unyayo.

 Mwigizaji wa sinema za Kibongo, Wastara Juma.

ATESEKA USIKU

“Alikuwa hapati usingizi usiku, ilibidi awe anakunywa dawa za kutuliza maumivu kila siku ndiyo aendelee na safari za kampeni kesho yake,” alisema ndugu huyo wa karibu wa Wastara.

AWASAKA MADAKTARI WAKE
Ndugu huyo alizidi kueleza kuwa, baada ya Wastara kumaliza kampeni, aliwasiliana na madaktari wake waliomtibu awali nchini Kenya ambao walimshauri awatumie picha ya eneo alilokuwa akisikia maumivu pamoja na mguu mzima wa baindia.

Madaktari hao baada ya kubaini mguu huo wa bandia umechoka na kusababisha tatizo la uvimbe, walimwambia anahitajika kukatwa sehemu ya mguu wake na kuwekewa mguu mwingine wa bandia.
“Aliwatafuta madaktari wake Kenya, wakamwambia hakuna ujanja kwa sehemu hiyo ilikuwa imevimba inatakiwa kukatwa ili aweze kuwekewa mguu mwingine,” alisema ndugu huyo.

WASTARA MWENYEWE

Baada ya kuzungumza na ndugu huyo, mwanahabari wetu alimtafuta Wastara mwenyewe ambaye alieleza kwa kirefu kuhusiana na tatizo hilo.“Unajua nilipokuwa kwenye kampeni, nilianza kusikia maumivu makali mno, nafikiri ni kutokana na kule kukimbiakimbia hivyo ilikuwa lazima ninywe dawa ya kupunguza maumivu kila wakati.

“Niliporudi ilibidi niombe ushauri kwa madaktari wangu ambao walinishauri niuchunguze vizuri mguu na niwatumie picha wao, nilipofanya hivyo niligundua mguu wangu wa bandia umekatika vidole viwili pia kwenye nyayo umeharibika sana,” alisema Wastara.

Mwigizaji huyo aliendelea kueleza kuwa tatizo hilo la kukatika vidole na nyayo kuharibika ndilo lililosababisha apate uvimbe ambao baadaye ulimfanya ashauriwe kukatwa kidogo ili kuwekewa mguu mpya wa bandia.

MILIONI TATU ZAHITAJIKA
“Hapa ninapokuambia mimi natakiwa milioni tatu kwa ajili ya kuweka mguu mwingine na nina maumivu makali sana yasiyopungua kila siku mpaka najiuliza hatma yangu jamani naumia.“Nipo katika mawazo sana, nikifikiria kukatwa tena mguu wangu yaani ni mateso juu ya mateso Mungu anisaidie kwa kweli maana mitihani hii kila siku mimi jamani,” alisema Wastara.

TUJIKUMBUSHE

Machi 12, 2009 wakati huo wakiwa wachumba tu, Wastara na marehemu Sajuki Juma, walipata ajali mbaya ya pikipiki maeneo ya karibu na walipokuwa wanaishi, Tabata, Dar es Salaam ambapo mwanadada huyo alivunjika mguu na kuharibika vibaya.

Baada ya hapo, Wastara alilazimika kukatwa mguu nchini Kenya na kuwekewa wa bandia kisha baadaye akafunga ndoa na marehemu mumewe, Sajuki.

Source:Global Publishers

0 comments: