Friday, 13 November 2015

Azam FC kuanzisha mradi mkubwa kuinua soka la vijana

 

TIMU ya Azam FC inatarajia kuanzisha mradi mkubwa wa kukuza soka la vijana unaojulikana kama ‘Azam FC Satelite Centre’.
Mradi huo utasimamiwa na Kocha Mkuu mpya wa Academy ya Azam FC, Tom Legg raia wa Uingereza, ambaye hivi karibuni alisaini mkataba wa miaka miwili kukinoa kikosi hicho.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, ameuambia mtandao wa azamfc.co.tz leo kuwa. lengo kubwa la mradi huo ni kuzalisha wachezaji bora vijana watakaopata nafasi ya kuingia kwenye academy (Azam FC) na wengine kusajiliwa na timu nyingine.
Alisema kwa kuanzia mradi huo utaanza na vituo vitano vitakavyokuwa kwenye mikoa mitano tofauti nchini, kwenye kila mkoa zitaundwa timu nne za vijana za chini ya miaka 10, 12, 14 na 16, huku akiongeza kuwa hadi kufikia mwaka 2025 wanataka wawe wamesambaza vituo hivyo nchi nzima.
“Katika kila kituo tutaajiri makocha wawili wazawa, daktari wa kutibu wachezaji na kiongozi wa kusimamia kituo. Makocha tutakaowachukua watapata mafunzo kutoka kwa kocha wetu wa academy na hao wengine nao tutawapa mafunzo kabla ya kuanza majukumu ya kusaka vipaji na kuunda timu,” alisema.
“Ni mradi mkubwa, ambao utaanza mara moja tutakapomaliza kuwapa mafunzo wataalamu hao,  utakuwa na manufaa kwa timu yetu na nchi kwa ujumla, kwa kuwa tutakuwa na uwezo wa kuzalisha vijana zaidi ya 600 kwa kuanzia watakaokuwa wakipata nafasi ya kucheza kwenye vituo vyote na baadaye watafikia 9,000, hivyo tutakuwa tumetengeneza njia ya vijana kupata nafasi ya kucheza.” alisema.
Kawemba alisema wachezaji wote wazuri watakaopatikana kupitia mradi huo, watapata fursa ya kujiunga na academy ya Azam FC kwa ajili ya kuongezewa ujuzi zaidi na hatimaye kupata nafasi ya kuchezea timu ya wakubwa.
“Kocha wa Academy atapata fursa ya kuzunguka siku nne hadi tano kwenye kila kituo kwa ajili ya kuwapa mafunzo na kuangalia namna programu inavyoendelea,” alisema.
Vijana kucheza Ligi
Kawemba alisema mara baada ya hatua ya kwanza kuisha ya kuvuna vipaji na wachezaji kupata mafunzo, katika hatua ya pili itaanzisha ligi ya vijana kwenye kila kituo itakayofanyika mara mbili kwa mwaka.
“Ligi hiyo itakuwa ikichezwa mara mbili kwa wiki, U-10 na 12 watacheza Jumamosi na U-14 na 16 watacheza Jumapili, kwenye kila mgawanyo wa umri kutakuwa na vijana 25, baada ya ligi hiyo kuchezwa mabingwa wote wa kila kituo kwa umri husika watakuja Dar es Salaam (Azam Complex) kucheza tena.
“Tunawaleta Dar es Salaam wakati shule zikiwa zimefungwa, ili waongeze bidii na watamani kucheza Azam FC, kufuatia kucheza kwenye miuondombinu mizuri, gym, bwawa la kuogelea, na mengine mengi, wakati huo tutatumia ligi ya hapa kuvuna vijana bora watakaobakia Azam Academy,” alisema.
Uongozi wa Azam FC pia umefungua milango kwa kuyakaribisha makampuni mbalimbali na nchini yanayotaka kushirikiana nao katika uendeshaji wa mradi huo kwa kudhamini, vilevile klabu zote nchini zinazotaka kujiunga nao.
Kocha Tom Legg anena
Naye Kocha mpya wa Academy, Tom Legg, alifurahishwa na mradi huo akisema utachochea maendeleo kwenye soka la Tanzania na Azam FC.
“Ni mradi mzuri sana, si timu nyingi Afrika zimepanga kufanya jambo kama hili, nimefanya kazi hii kubwa nikiwa hapa Afrika katika nchi ya Sierra Leone, nimesaidia sana kuinua kiwango chao cha soka, kwani nchi hiyo ilipanda kwa nafasi 20 kwenye viwango Fifa kutoka 50 hadi 70, lakini baada ya kuondoka hivi sasa wanapotea,” alisema.
“Programu kama hizi zinahitaji muda, naamini baada ya miaka mitano tutaanza kupata wachezaji wazuri, ambao hawatakuwa na mchango ndani ya Azam FC tu bali kwa Tanzania nzima,” alisema.
Legg amefurahishwa sana na miundombinu ya Kituo cha Azam Complex kutokana na ubora wa hali ya juu na kusema kuwa angependa kuona wachezaji wa vituo vitakavyoanzishwa wanapata nafasi ya kufika kwenye kituo hicho ili kuwahamasisha wawe na malengo ya kufika hapo.
Legg, 28, ni kocha mzoefu mwenye elimu ya daraja A la Baraza la Vyama vya Soka Ulaya (UEFA), aliyefanya kazi kwenye klabu kubwa barani Ulaya, America Kaskazini, Asia na Afrika.
Amewahi kufanya kazi barani Asia katika nchi ya Cambodia, akiwa kama Mkurugenzi wa Ufundi wa Academy ya timu ya Phnom Penh Crown, pia Kocha Mkuu wa Kituo cha Craig Bellamy Foundation cha Sierra Leone kuanzia Mei 2012 hadi Oktoba 2014.
Kocha huyo kijana pia amewahi kufanya kazi kama Mkuu wa Kutathmini Viwango vya Wachezaji wa timu ya Taifa ya Sierra Leone kuanzia Juni 2013 hadi Oktoba 2014.

0 comments: