Saturday, 21 November 2015

Wanachama 115 wa CHADEMA na CUF Wahamia CCM Wilayani Handeni Mkoani Tanga


 

Wanachama 115 wa Chadema na CUF wilayani Handeni Mkoa wa Tanga, wamejiunga na CCM kwa madai kuwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umeshindwa kuelewana hadi kipindi cha Uchaguzi Mkuu.

Wakirudisha kadi na bendera juzi mbele ya Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Tanga, Mathew Mganga walisema walikuwa na nia ya kweli ya kuunga mkono Ukawa unaoundwa na vyama vyao lakini kutokana na kutokuwa na msimamo wameamua kuhama.

Katibu wa Chadema Kata ya Kwenjugo, Rajabu Vuli, alisema alifanya hamasa kuhakikisha chama chao kinapata ushindi lakini viongozi wa wilaya hawakuonyesha ushirikiano na watu wa chini.

Mwingine aliyehama ni Katibu wa Vijana wa Chadema wa kata hiyo, Ramadhani Dawa.

Dawa alisema ahadi zisizotimia za viongozi ikiwamo kuwadharau viongozi wa kata ndiyo sababu kubwa iliyosababisha kuhamia CCM.

Alisema kama wasingedharauliwa na mawazo yao kufanyiwa kazi wangebaki Chadema na kukiendeleza chama hicho ambacho amedai kimekuwa na mvuto mkubwa na Watanzania ambao walitaka kuleta mabadiliko ya kweli.

Mganga alisema wamepokea wanachama hao bila wasiwasi kwani tayari hizo ni kura.

Hivi sasa chama hicho kipo kwenye kampeni za kumuombea kura mgombea ubunge Jimbo la Handeni Mjini (CCM), Omari Kigoda.

Alisema wameridhika na uamuzi wa wanachama hao wapya kwa kuona CCM inajali ngazi zote za uongozi kuanzia wa chini hadi juu.

Alisema baada ya uchaguzi huo mdogo, watahakikisha yale walioahidi kwa wananchi yanafanyiwa kazi haraka hasa yanayowagusa moja kwa moja ikiwamo elimu, afya, maji na masuala ya miundombinu.

Mgombea ubunge huyo, aliahidi endapo atapewa ridhaa ya kuongoza jimbo hilo, atawaleta maendeleo.
 

0 comments: