Thursday, 19 November 2015

Mama Amchoma Mwanaye Kwa Maji Moto Baada ya Kumtuhumu Ameiba Nyama Jikoni

 
 Polisi mkoa wa Mara inamshikilia mwananke mmoja (jina tunalo) mkazi wa Bweri Manispaa ya Musoma kwa kosa la kumchoma mtoto wake mwenye miaka minne, kwa maji ya moto, mikono yote miwili baada ya kumtuhumu kuwa ameiba nyama jikoni.

Mama huyo alikamatwa Novemba 14 saa nne asubuhi katika eneo la Morembe kata ya Bweri mjini Musoma baada ya Polisi kufika nyumbani kwake kumkamata kwa kosa jingine la kumkatakata kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili Kabula Rubeni (32) akimtuhumu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mume wake.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mara, ACP Alex Philip Kallangi alidai kuwa siku ya tukio hilo la kumchoma moto mtoto huyo, mama yake mzazi alikuwa amepika nyama jikoni na baadaye alikwenda kuchota maji.

Kamanda Kallangi alidai baada ya mama huyo kurudi alimkuta mwanaye anakula nyama ndipo alishikwa na hasira na kuanza kumchapa sehemu mbalimbali za mwili wake na kisha akachukua mikono yote miwili na kumchoma kwa maji ya moto.

Baada ya kufanya kitendo hicho cha kinyama, mama huyo alianza kumtibu mtoto huyo kwa siri hapo nyumbani kwa dawa za kienyeji bila majirani kufahamu kilichokuwa kikiendelea nyumbani kwa mama huyo.

Kamanda Kallangi alieleza kuwa kilichosababisha kufahamika kwa taarifa hizo, ni baada ya Kabula aliyekuwa ameshambuliwa kwa mapanga na mwanamke huyo kwenda polisi kutoa taarifa ya kushambuliwa.

Kallangi alieleza kwamba polisi walipofika nyumbani kwake ndipo walipewa taarifa za mtoto huyo kujeruhiwa kwa kuchomwa moto. Kutokana na tukio hilo polisi hao, kwa kushirikiana na maofisa ustawi wa jamii na kituo cha ushauri cha Jipe Moyo walimchukua mtoto huyo na kumpeleka katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara kwa matibabu na kisha kupelekwa Jipe Moyo anakoishi hadi sasa kwa uangalizi zaidi.

Kallangi alisema mtuhumiwa huyo yupo kituoni na anatarajiwa kufikishwa mahakamani hivi karibuni kujibu mashtaka yanayomkabili.

Ofisa Ustawi wa Jamii Musoma, Vedastus George aliwataka wazazi na walezi kuzuia hasira zao pale watoto wanapowakosea na hata wanapowaadhibu wawe makini ili waziwaumize kama alivyofanyiwa mtoto huyo.

0 comments: