Friday, 13 November 2015

Sasa kumecha Rais Magufuli Kuteua Wabunge Muda Wowote Kuanzia Sasa

 

Rais John Magufuli anatarajiwa, wakati wowote kuanzia sasa, kuwateua baadhi ya watu wenye sifa kuwa wabunge ili aweze kuwapa majukumu ya kuongoza wizara atakapopanga safu ya Baraza la Mawaziri, hivi karibuni.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inampa Rais mamlaka ya kuteua wabunge wasiozidi 10 kutoka miongoni mwa wananchi ambao anaona wanaweza kumsaidia katika utekelezaji wa majukumu yake katika baadhi ya maeneo kama vile afya, elimu, kilimo, nishati na sheria.

Ibara ya 66 (1) inasema, bila ya kuathiri masharti mengine ya ibara hii, kutakuwa na aina zifuatazo za wabunge, yaani (e) wabunge wasiozidi 10 walioteuliwa na Rais kutoka miongoni mwa watu wenye sifa kwa mujibu wa ibara ya 67, isipokuwa sifa iliyotajwa katika ibara ya 67(1) (b).

Baraza hilo jipya linatarajiwa kuwa na sura nyingi mpya ambazo zitaendana na kasi yake kutekeleza kaulimbiu ya “Hapa Kazi Tu.” Pia, baraza litakuwa na sura mpya kutokana na ukweli kwamba baadhi ya mawaziri waliangushwa kwenye kura za maoni, wengine wakati wa Uchaguzi Mkuu na wengine, japokuwa wamerejea bungeni ni walionekana kuwa mzigo awamu iliyopita.

Kati ya mawaziri 55 waliokuwamo katika Baraza lililopita, waliorejea katika Bunge la 11 ni 23 tu wakiwamo 20 wa majimbo na watatu wa viti maalumu. Kupungua kwa idadi hiyo kutampa Dk Magufuli fursa ya kusuka baraza hilo kutoka miongoni mwa wabunge 188 wa majimbo, 64 wa viti maalumu na 10 atakaowateua ili wamsaidie.

Haijulikani baraza litakuwa na mawaziri wangapi ila wakati wa kampeni amewahi kukaririwa akisema litakuwa dogo ikilinganishwa na lililopita.

Katika muhula wa pili wa utawala wake, Rais Kikwete aliwateua wabunge 10, kati yao sita aliwapa wizara za kuongoza, utaratibu ambao huenda Dk Magufuli akautumia ili kupata mawaziri kulingana na mahitaji ya Serikali atakayoiunda.

Kwanza Rais Kikwete alimteua Profesa Makame Mbarawa na akamfanya Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia; na Shamsi Vuai Nahodha ambaye alipewa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Pia, alimteua Zakhia Meghji lakini hakumpa wizara, na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia (sasa mbunge mteule wa Vunjo).

Baada ya kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri mwaka 2012, Rais Kikwete aliwateua Profesa Sospeter Muhongo (sasa mbunge mteule wa Butiama) akampa Wizara ya Nishati na Madini; Janet Mbene na Saada Salum Mkuya akawafanya manaibu waziri katika Wizara ya Fedha. 

Janet ambaye baadaye aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara ameshinda ubunge katika Jimbo la Ileje na Mkuya anasubiri hatima yake katika Jimbo la Kijitoupele, Zanzibar. Aidha, alimteua Dk Asha-Rose Migiro kuwa Waziri wa Katiba na Sheria na hivi karibuni alikamilisha orodha kwa kuwateua Dk Grace Puja na Innocent Sebba.

Baraza la Mawaziri litajulikana baada ya wabunge kula kiapo wiki ijayo mbele ya Spika wa Bunge ambaye anatarajiwa pia kuchaguliwa wiki ijayo.
 

0 comments: