Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amefichua mazito baada ya kueleza hadharani kuwa kamwe chama chake na washirika wao wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) hawatakubali matokeo ya uchaguzi mkuu yatakayobainika kuwa yamepikwa.
Kadhalika, alisema ni vyema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na mamlaka za serikali iliyopo madarakani kuheshimu maamuzi ya wananchi yatakayotokana na kura watakazopiga kwenye uchaguzi mkuu Jumapili ijayo, kwani kinyume chake ni kuhatarisha amani iliyopo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana baada ya kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Dk. Emmanuel Makaidi wa chama cha National League for Democracy (NLD) aliyefariki dunia wiki iliyopita, Mbowe alisema watakubali matokeo ikiwa mchakato wote wa uchaguzi utakuwa huru, wa haki na usiokuwa na chembe ya mizengwe katika kila hatua.
Chadema na vyama vingine vinavyounda Ukawa vya Chama cha Wananchi (Cuf), NCCR-Mageuzi na NLD, vimemsimamisha waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuwa mgombea wao wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku pia wakishirikiana kusimamisha wagombea wa nafasi za ubunge, udiwani na uwakilishi.
Akieleza zaidi, Mbowe aliyekuwa akijibu swali aliloulizwa na waandishi kuhusu namna walivyojiandaa kupokea matokeo baada ya uchaguzi mkuu Jumapili ijayo, alisema Ukawa itakuwa tayari kupokea matokeo yatakayotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ikiwa wataridhika kuwa hatua zote za kisheria na haki za mchakato wa uchaguzi huo kuanzia katika kampeni hadi upigaji kura zimezingatiwa ipasavyo.
Aliongeza kuwa kinyume chake, wao (Ukawa) hawatakuwa tayari kupokea matokeo yatokanayo na hila za namna yoyote ile.
Akifafanua, Mbowe alisema Ukawa haiwezi kukataa matokeo kwa sababu ya kushindwa katika uchaguzi, bali wanachoangalia ni kuzingatiwa kwa haki, sheria na uwazi katika hatua zote za mchakato wa uchaguzi huo.
“Kupokea matokeo ni mchakato ambao unaanzia katika hatua za kampeni, upigaji kura hadi wakati matokeo yanatangazwa. Siwezi kusema eti tutakataa matokeo kwa sababu tu Nec imetangaza halafu tukaonekana tumeshindwa… la hasha. Bali tutapokea matokeo kama haki, uwazi, sheria na taratibu nyingine zimezingatiwa mpaka kupatikana kwa matokeo,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Sisi Chadema na Ukawa tunaamini kwamba wananchi watamchagua kiongozi wanayemuamini. Lakini kama watu wengine wenye mamlaka ndani ya nchi wakaamua kupindisha sheria na kupindisha maamuzi ya wananchi kupitia sanduku la kura, kamwe hatutakubali matokeo hayo. Na hapo amani tunayoihubiri inaweza kuwa ngumu ‘kui-control’ (kuidhibiti),” alisema.
Kuhusiana na mvutano juu ya wananchi kuondoka vituoni baada ya kupiga kura na siyo kukaa mita 200 kutoka kwenye vituo vya kura, Mbowe alisema msimao wao wa kulinda kura uko pale pale kwa kuwa wana amini kuwa hiyo ni haki yao kisheria.
“Kura ni mali na kama hivyo ndivyo ni lazima tuilinde, tumepanga kulinda kura zetu kwa amani na utulivu nje ya mita 200 kama sheria inavyosema… tunaomba kila mtu na vyombo vya dola viheshimu,”alisema.
Aliongeza: “Kuhubiri amani bila haki ni kulishana upepo. Mamlaka zote za taifa zina wajibu wa kuheshimu sheria za nchi na kuacha kutumia mamlaka zao vibaya na bila vitisho. Kila mmoja akitekeleza wajibu wake kwa misingi ya sheria, hiyo amani wala haitatafutwa, itapatikana tu.”
Mbali na Mbowe, wengine waliojitokeza katika shughuli ya kuuaga mwili wa Dk. Makaidi ni Lowassa, Mgombea Mwenza wa Ukawa, Juma Duni Haji, Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia wa NCCR-Mageuzi , Waziri Mkuu Mstaafu aliyehamia kambi ya Ukawa, Frederick Sumaye, Kaimu Katibu Mkuu wa Cuf, Twaha Tasilima, Katibu Mkuu wa NLD, Tozzy Matwanga na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula.
Wengine waliokuwapo ni Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, mgombea ubunge wa Jimbo la Kawe, Halima Mdee.
Jaji Mkuu Ataka Mahakama Iachiwe Swala la Mita 200
Wakati Mbowe akisisitiza msimamo wa kuwataka wafuasi wa Ukawa kutorudi nyumbani baada ya kupiga kura na badala yake kukaa umbali wa mita 200 kutoka vituo vya kupigia kura ili kulinda kura zao, Jaji Mkuu Othman Chande alikataa kuzungumzia suala hilo na badala yake kutaka mahakama iachiwe ili itoe uamuzi wake kwa haki.
Jaji Chande aliyasema hayo jana wakati alipoulizwa na waandishi baada ya kufungua mafunzo kwa majaji na Wasajili Mahakama Kuu Jijini Dar es Salaam, juu ya wajibu wa mahakama katika uchaguzi mkuu na namna ya kukabiliana na changamoto zilizopo katika kusimamia kesi za uchaguzi, yaliyoandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC).
Tayari Mahakama Kuu imeshapanga majaji watatu kushughulikia suala hilo lililoibua mvutano mkali hivi karibuni baina ya viongozi wa Ukawa na wakuu wa Nec na Jeshi la Polisi. Kesi hiyo itaanza kunguruma rasmi leo.
Katika hatua nyingine, Jaji Chande alikiri kuwa uchaguzi wa mwaka huu ni wenye mchuano mkali na kwamba mahakama zimejiandaa kumaliza kesi zitakazotokana na uchaguzi huo kabla ya miezi sita inayotajwa kisheria.
Alisema mwaka 2010 kulikuwa na kesi 44 za uchaguzi kwa ngazi za Ubunge na kati yake, 17 zilikwenda hadi hatua ya mwisho baada ya kutolewa ushahidi huku nyingine zikiisha katika hatua za awali.
“Ushindani ni mkali katika uchaguzi huu, tunatarajia kupokea kesi nyingi za uchaguzi. Tumejiandaa kupokea, kusikiliza kwa haraka ili kuwezesha wapigakura kujua mshindi halali ni yupi,” alisema.
Akieleza zaidi, alisema sheria imeweka wazi kuwa anayestahili kufungua kesi siyo mpigakura bali wagombea wenyewe.
Mratibu THRDC, Onesmo Olengurumwa, alisema wameshirikiana na Ofisi ya Jaji Kiongozi kuandaa mafunzo hayo kwa kutambua kuwa ni wadau muhimu katika kushughulikia kesi za uchaguzi ili kuwezesha haki kutendeka kwa haraka
0 comments:
Post a Comment