Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli.
Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema amepata taarifa kwamba kuna njama zinaandaliwa kwa lengo la kumuangusha mgombea ubunge Jimbo la Mtama kwa tiketi ya chama hicho, Nape Nnauye.
Dk. Magufuli aliyasema hayo jana wakati akizungumza kwenye mkutano wa kampeni katika Jimbo la Mtama mkoani Lindi.
Alisema Nape anaandaliwa njama ili asipite katika kinyang’anyiro cha ubunge jimboni humo kwa sababu aliwataka baadhi ya wana-CCM wajivue gamba wakati chama hicho kikiwa katika mchakato wa kufanya mabadiliko.
Hata hivyo, Dk. Magufuli alisema Nape ni kiongozi mzuri ambaye endapo yeye (Dk. Magufuli), angekuwa na uwezo wa kumhamisha, angemhamishia kwenda kugombea katika jimbo lake la Chato.
“Nape amekuwa jasiri kuwasema wezi serikalini na ndiyo maana anaandamwa ili wamwangushe…..sasa kwa sababu mimi ndiye nitakuwa rais kwa vyovyote vile, namtaka Nape ili nifanye naye kazi….wananchi msikubali hila hizo nataka mmlete huyu,” alisema Dk. Magufuli.
Aidha, Dk, Magufuli alisema anawapenda wanachama wa vyama vya upinzani wakiwamo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwa sababu anajua nao wanampenda na watampigia kura kwa wingi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Alisema matatizo yaliyoko kwenye jamii kama maji na umeme, yanawagusa wananchi wa vyama vyote vya siasa, hivyo aliwaomba waweke pembeni masuala ya vyama na wamchague yeye kuwa rais wa awamu ya tano.
Alisema rais anayehitajika ni yule atakayeleta mabadiliko ya kweli na kwa kasi kubwa na si kwa mbwembwe za kuzungusha zungusha mikono kama wanavyofanya wagombea wa upinzani wanapojinadi.
NA JOSEPH MWENDAPOLE
0 comments:
Post a Comment