Tuesday, 20 October 2015

Ikitokea Lowassa Akashindwa! Mwana CCM Yeyote Atakaembeza Lowassa Kutokana na Kushindwa Huko Atakuwa ni "Mpumbavu na Zuzu


LOWASSA ATABAKI KUWA SHUJAA WA MABADILIKO..!!
Nikiwa mwanachama wa CCM imenipasa kuamini kuwa chama changu kitashinda uchaguzi huu. Pamoja na imani hii sitashangaa kama CCM yangu itaanguka ingawa nitasikitika. Ikitokea, Mh. Lowassa akashindwa katika uchaguzi huu; mwana CCM yeyote atakaembeza Mh. Lowassa kutokana na kushindwa huko atakuwa ni "mpumbavu na zuzu". 
Kwa nini? Ni kwa sababu chama chetu CCM kilijisahau mno na kilishafika hatua ya kuwa na kiburi cha madaraka(na ndio maana mgombea wetu kaamua kujinadi kwa jina lake badala ya jina la chama kutokana na wananchi wengi kukasirishwa na mwenendo wa baadhi ya waliopewa dhamana ya kuongoza serikali kwa mgongo wa chama na chama kuonekana hakifai)! Kimsingi hakukuwa na namna yeyote ya kukizindua CCM na kukishikisha adabu zaidi ya kutokea kwa ushindani kama huu aliouleta Mh. Lowassa na UKAWA kwa ujumla

Kampeni zinapoanza CCM sio tu ilibeza mabadiliko bali pia ilitumia muda mwingi kuwatukana wapiga kura wanaotaka mabadiliko(nikiwemo mimi mwanachama wake); lakini hadi sasa kumekuwa hakuna jinsi zaidi ya kuhubiri na kutafutia kura kwa jina la mabadiliko ya kweli. Kutokana na rekodi za kiutendaji zilizotukuka na uwezo wake binafsi natumaini Magufuli anaweza kushinda(ushindi wa kawaida na sio wa kishindo).

 Lakini ikitokea Mh. Lowassa ameshindwa, mimi sitahesabu kama ameshindwa bali nitamweka kwenye kumbukumbu ya mashujaa waliolazimisha mabadiliko katika wakati sahihi. Mwanachama anaekitakia mema CCM huko mbeleni, atakuwa mvivu wa kufikiri asipompongeza Mh. Lowassa kwa mabadiliko ya kweli yanayotegemewa kuletwa na Dk. Magufuli pindi achaguliwapo kuwa Rais wa JMT. Kwa maana bila "mziki" wa Lowassa kutikisa nchi, CCM ilishashupaza shingo kukubali kuwa wananchi wamechoka tambo za kuimba eti, "CCM ni ile ileeeee...." bali wananchi na wanachama(hasa wa zama mpya) tunataka mabadiliko. 

Hivyo basi, kutokana na mwenendo wa kampeni hadi sasa nimejiridhisha kuwa hata Dk. Magufuli anao uwezo wa kwenda kinyume na mfumo na kuleta mabadiliko[kama akiamua kuwaua nyani pasipo kuwaangalia usoni], [maana ni yeye aliewazindua wenzie pale juu; kuwa ikiwa wataendelea kubeza mabadiliko basi CCM itaanguka mchana kweupe!]. Kwa hiyo ukiamua kumpa kura yako Dk. Magufuli, mpe tu bila wasiwasi! ~SmartVoter~

0 comments: