Friday, 23 October 2015

ELIMU YA STADI ZA MAISHA KUOKOA KUNDI KUBWA LA VIJANA WALIO NJE YA SHULE


unnamed
Afisa vijana kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bw. Godfrey Massawe (aliyesimama) akifuatilia majadiliano ya wawezeshaji kitaifa wakati wa kazi za kikundi kwenye Mafunzo ya Uwezeshaji wa Stadi za Maisha yaliyofanyika Kanda ya Ziwa.

………………………………………………………………………………….
Na: Genofeva Matemu – Maelezo
Iligundulika kuwa ulimwenguni kote na hususan nchini Tanzania, Vijana walio nje ya shule ni miongoni mwa makundi yaliyo katika hatari ya magonjwa yanayoenea kwa njia ya ngono, VVU na UKIMWI kwa kutokuwa na taarifa na stadi za kuwaongoza hivyo kupoteza kundi kubwa la vijana ambalo ni taifa la kesho.
Ufumbuzi wa tatizo hili umeweza kufanyika kwa kuwapa vijana stadi za maisha zenye upeo mpana wa maarifa na stadi zinazoweza kuwasaidia vijana kuendana na mazingira shindani yanayobadilika.
Stadi za maisha ni moja kati ya mikakati iliyobainika kuleta mabadiliko ya tabia za mtu. Stadi hizi uhusisha stadi na uwezo wa kujenga tabia njema ili kuepukana na matatizo yaliyopo katika maisha ya kila siku.
Mkabala wa stadi za maisha unalenga katika kuendeleza na kukuza stadi zinazoitajika katika mahitaji ya maisha ya kila siku kama vile mawasiliano, kufanya maamuzi, fikra, kuhimili mihemko, uthubutu, ujenzi wa kujiamini, kuzuia shinikizo rika pamoja na mahusiano.
Mkabala huu pia unashughulikia ukuaji wa mtu ili awe na stadi za kumwezesha kutumia aina zote za taarifa kuhusiana na masuala kama vile magonjwa ya ngono, VVU na UKIMWI.
Mahitaji ya stadi za maisha miongoni mwa vijana ni mengi na yanatofautiana baina ya vijana wadogo na wakubwa, vijana walio nje ya shule na walio shuleni, pamoja na walio na wasio katika ndoa hivyo kupelekea kuwa na viwango vya mafunzo ya stadi za maisha vilivyopendekezwa na kubuniwa kuwanufaisha vijana wasio mashuleni.
Wizara inayosimamia masuala ya vijana imekua ikitoa mafunzo ya stadi za maisha kwa vijana walio nje ya shule ili kuwapa vijana stadi za kukabiliana na changamoto za kila siku katika maisha yanayowazunguka.
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa kushirikiana na shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA) wameweza kufikisha elimu ya stadi za maisha kwa wawezeshaji wa kitaifa kutoka kanda ya Ziwa hivi karibuni ili kuweza kusambaza elimu hiyo kwa vijana walio nje ya shule maeneo yote ya kanda ya ziwa hivyo kuwawezesha vijana kukabiliana na dunia hii ya sasa ya sayansi na teknolojia.

0 comments: