Sunday, 10 April 2016

ESPERANCE AFA CHAMAZIKIMYAKIMYA MAMBO YA FARID NA ‘MESSI’ 2-1


Farid Mussa shujaa wa Azam leo

AZAM FC imejiweka kwenye nafasi ya kwenda hatua ya mchujo wa kuwania kupangwa kwenye makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Hiyo inafuatia ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Esperance ya Tunisia jioni ya leo katika mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Shukrani kwao, wachezaji vijana wadogo Farid Mussa Malik na Ramadhani Yahya Singano ‘Messi’ waliofunga mabao hayo kipindi cha pili baada ya Azam FC kuwa nyuma kwa 1-0 tangu kipindi cha kwanza.
Azam FC inayomilikiwa na Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake sasa inatakiwa kwenda kulazimisha sare yoyote ugenini katika mchezo wa marudiano wiki ijayo ili kwenda hatua ya mwisho ya kuwania kucheza hatua ya makundi.
Esperanace walipata bao lao dakika ya 33 kupitia kwa Haithem Jouini aliyefunga kwa kichwa akimalizia krosi ya Ilheb Mbaark.
Nahodha John Bocco alipoteza nafasi zaidi ya mbili za wazi kipindi cha kwanza, ikiwemo dakika ya 22 baada ya kupiga nje akiwa amebaki yeye na kipa.
Mshambuliaji mwingine tegemeo wa Azam, Kipre Herman Tchetche alipoteza nafasi nzuri dakika ya 36 baada ya kupiga juu akiwa mbele ya lango.
Kipindi cha pili, mabadiliko yaliyofanywa na kocha Muingereza Stewart Hall kumtoa kiungo Muivory Coast, Kipre Michael Balou na kumuingiza mzawa, Frank Raymond Domayo yalirejesha uhai kwenye kikosi cha Azam.
Na hapo ndipo Azam FC walipofanikiwa kubadilisha na matokeo ya mchezo pia kutoka kuwa nyuma kwa 1-0 hadi kuongoza kwa 2-1.
Farid alianza kufunga dakika ya 68 baada ya kutanguliziwa pasi fupi na Singano Messi.
Kiungo wa zamani wa Simba, SIngano ‘Messi’ akaifungia bao la ushindi Azam dakika ya 70, safari hiyo naye akisetiwa na Farid Mussa kwa krosi nzuri kutoka upande wa kushoto.
Esperance walionekana kupagawa na mabao hayo mawili ya haraka na kuwaruhusu Azam kuongeza mashambulizi langoni mwao.
Kiungo wa Azam FC, Farid Mussa (kulia) akimtoka beki wa Esperance, Yacine Rabii
Mshambulkiaji wa Azam FC, Kipre Herman Tchetche akipambana katikati ya wachezaji wa Esperance, Ilyes Jelassi (kushoto) na Mobamed Yaakoubi 

Beki Muivory Coast, Serge Wawa alishindwa kuendelea na mchezo dakika ya 89 baada ya kuumia misuli na nafasi yake kuchukuliwa na David Mwantika aliyemalizia mchezo vizuri.
Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Waziri Salum/Khamis Mcha ‘Vialli’ dk67, Aggrey Morris, Serge Wawa/David Mwantika Serge Wawa dk89, Jean Baptiste Mugiraneza, Kipre Tchetche, Kipre Bolou/Frank Domayo dk46, Ramadhani Singano ‘Messi’, John Bocco na Farid Mussa.
Esperance: Moez Ben Cherifia, Iheb Mbaarki, Yacine Rabii, Mohamed Ali Yaakoubi, Chamseddine Dhaouadi, Hoiucine Regued, Fousseny Coulibaly, Driss Mhirsi, Ilyes Jelassi/Adem Rjaibi dk75, Fakhreddine Ben Youssef na Haithem Jouini



Na Somoe Ng'itu, DAR ES SALAAM

0 comments: