Wednesday, 4 November 2015

Mgawanyo Viti Maalum Bunge la 11 Kwa Kila Chama



Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 Nec, ilitenga viti 102 kwa ajili ya Wabunge Wanawake, ikiwa ni sawa na asilimia 40 ya Wabunge 256 waliokuwapo (majimbo 239 na 17 wengineo).

Katika uchaguzi huo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilipata wabunge 69 na vyama vingine CUF na Chadema viti 33.


Katika mchakato huo, idadi ya Viti Maalum kwa CCM itapungua huku ya vyama vya upinzani ikizidi kuongezeka kutokana na uwapo wa wagombea wake kila jimbo.

Ili chama kipate viti maalum ndani ya Bunge la 11, ni lazima kiwe na asilimia tano ya kura za ubunge nchini nzima.

Kwa kutimiza sifa hiyo, ni dhahiri kuwa vyama vitakavyopata Viti Maalum ni CCM, Chadema na CUF kutokana na idadi ya kura za ubunge kwa kila jimbo.

Idadi ya Viti Maalum kwa CCM itapungua tofauti na vipindi vilivyopita kutokana na vyama vya upinzani kama Chadema, CUF na ACT kusimamisha wagombea katika majimbo yote nchini na hivyo kupunguza kura ambazo chama hicho tawala kingezipata katika majimbo.

Katika uchaguzi wa mwaka huu uliohusisha majimbo 258 kati ya 264, CCM imeshinda ubunge katika majimbo 182, ikifuatiwa na CUF iliyoshinda katika majimbo 39 na Chadema 35, huku vyama vya ACT-Wazalendo na NCCR- Mageuzi vikipata kiti kimoja kimoja.

Majimbo nane hayajafanya uchaguzi wa wabunge kutokana na sababu za vifo vya wagombea katika majimbo sita na kasoro mbalimbali katika majimbo mawili.

Majimbo ambayo wagombea walifariki dunia ni Ludewa, Lushoto, Ulanga Mashariki, Arusha Mjini, Handeni Mjini na Masasi. Majimbo yenye kasoro ni Lulindi na Kijitoupele.

Bunge la 10 kulikuwa na wabunge wa majimbo 254, kati yake CCM ilikuwa na viti 186, CUF 23 na Chadema 24, NCCR-Mageuzi vinne huku UDP kiti kimoja na TLP kimoja. Wa kuteuliwa na rais kumi, Baraza la Wawakilishi watano.

Licha ya Chadema kuwa na wabunge wachache wa majimbo ikilinganishwa na CUF, lakini itakuwa na wabunge wengi wa Viti Maalum kutokana na wingi wa wapiga kura wa majimbo ya bara ambayo Chadema imeshinda katika nafasi hiyo.

HESABU ZINAVYOPIGWA
Ili kupata viti maalum kwa kila chama ni lazima ijulikane idadi ya viti hivyo kwa kipindi hiki ambacho ni sawa na asilimia 30 ya wabunge 281 ambayo ndiyo wabunge wa Bunge lijalo.

Kwa hesabu hizo, viti vya Wabunge Maalum vitakuwa kati ya 84 au 85 ikilinganishwa na vya Bunge lililopita ambalo vilikuwa 102.

Chanzo kimoja kimeieleza Nipashe kuwa kwa hesabu hizo, CCM itapata viti 46. Bunge lililopita chama hicho kilikuwa na Viti Maalum 69.

Kwa mujibu wa Katiba idadi ya wabunge wanawake (Viti Maalum) isipungue asilimia 30 ya wabunge wote waliotajwa katika Katiba.

Kwa mujibu wa kilichoandikwa katika ukurasa wa ‘Facebook’ wa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Ummy Mwalimu, wabunge wanaohesabiwa ni wa majimbo 264, Baraza la Wawakilishi watano, Mwanasheria Mkuu wa Serikali mmoja, uteuzi wa Rais 10 na Spika kama sio mbunge mmoja na kufanya jumla ya 281.

“Hivyo katika Bunge hili, Wabunge V/Maalum wanatakiwa wasipungue asilimia 30 ya Wabunge 281,” alieleza.

Mwalimu alifafanua kuwa upatikanaji wake wanachaguliwa na vyama vya siasa kwa kuzingatia masharti ya uwiano wa kura ambazo kila chama kimepata katika uchaguzi wa Wabunge na siyo idadi ya wabunge. “Kila kura moja inachangia kupatikana kwa wabunge Viti Maalum. Wataalamu wa mifumo ya uchaguzi wanautambua mfumo huu kama ‘proportional representation’. Tofauti na mfumo wa uchaguzi wa wabunge wa majimbo ambao ni ‘Aliyepata kapata na aliyekosa kakosa,” alifafanua katika ukurasa huo.

Mwalimu ambaye ni mshindi wa Viti Maalum mkoani Tanga, amefafanua kuwa kama chama kimepata kura halali za Wabunge asilimia 60 basi kitapata asilimia 60 ya viti vilivyotengwa.

0 comments: