MCHEZO MZURI,MATOKEO MABAYA..!
TAARIFA HII NI KWA MIJBU WA WEBCITY YA MBEYA CTY
Imekuwa ni siku mbaya kwa wachezaji, mashabiki na wadau wa Mbeya City Fc, kufuatia kupoteza mchezo wa jana wa ligi kuu ya soka Tanzania bara dhidi ya Simba ya Dar es Salaam uliochezwa kwenye uwanja wa Sokoine jijini hapa.
Bao la mapema katika dakika ya 4 ya kipindi cha kwanza lililofungwa na mlinzi Juuko Mursheed lilitosha kuipa timu hiyo ya Dar ushindi wa kwanza mbele ya City baada ya misimu miwili ya tabu tangu timu hizi zilipokutana kwa mara ya kwanza mwaka 2013/14 na kuanza kwa sare kwenye mchezo wa kwanza.
Katika mchezo wa jana Simba walikianza kipindi hicho cha kwanza kwa kasi kubwa wakilishambulia lango la City kwa pasi za haraka haraka na kufanikiwa kupata kona ndani ya dakika hizo nne, kona hiyo ilipigwa kiufundi na mlinzi Hassan Kessy na kumkuta mfungaji aliyekuwa amesimama kwenye nguzo ya mwisho, jitihada za mlinzi Christian Sembuli hazikutosha kuuokoa mpira uliokuwa umegongwa kwa kichwa na Mursheed.
Kuingia kwa bao hilo kuliiamsha City na kuanza kucheza mpira safi wa pasi fupi fupi huku safu ya kiungo iliyokuwa ikiongozwa na Steve Mazanda, Rafael Daud na Christian Sembuli ikitawala eneo hilo kwa kiasi kikubwa,Temi Felix nusura aipatia timu yake bao la kusawawisha katika dakika 20 kufuatia kuunganisha vizuri mpira wa krosi uliopigwa na Hasani Mwasapili kutoka upande wa kushoto lakini Shuti lake liliokolewa na kipa wa Simba Vincent Agban.
City iliendelea kucheza vizuri na kutawala mchezo huo kwa kipindi chote cha kwanza licha ya Simba kuzinduka mara chache na kufanya mashambulizi ya kushtukiza lakini uimara wa walinzi pande zote mbili ulifanya dakika 45 za kwanza kumalizika matokeo yakibaki bao 1 kwa Simba na City wakiwa hawana bao.
Kipindi cha pili kocha wa City, Abdul Mingange alifanya mabadiriko kadhaa kwa kumtoa Christian Sembuli na kuingia Abdalah Seif pia aliwatoa Haruna Moshi na Rafael Daud na nafasi zao kuchukuliwa na Hamad Kibopile na Geofrey Mlawa mabadiliko ambayo yalizidi kuiimarisha timu na kuendelea kuishambulia Simba kwa muda wote wa kipindi hicho.
Mshambuliaji Geofrey Mlawa ataukumbuka mchezo huu kufuatia kushindwa kutumia vizuri nafasi mbili za wazi alizopata kwenye dakika ya 41 na 44 za kipindi hicho cha pili akiwa ndani ya eneo la hatari la Simba lakini mara zote alipiga mipira iliyowababatiza walinzi na kipa Agban na kuokolewa hivyo kukamilisha dakika 90 City ikiwa nyuma kwa bao hilo moja.
Mara baada ya mchezo kocha Abdul Mingane aliwashukuru wachezaji wake kwa kucheza vizuri huku akisikitishwa na umakini mdogo kwenye safu ya ushambuliaji ambayo licha ya kupata nafasi nyingi ilishindwa kuweka mpira kimiani.
“Nashukuru, tumecheza mpira mzuri lakini umakini kwenye safu ushambuliaji umetufanya kukosa ushindi, haya ni matokeo mabaya ambayo yanamsikitisha kila mmoja lakini soka ndivyo ilivyo, tunarudi kambini kujiandaa na mchezo mwingine kitu muhimu kwetu ni kujiweka vizuri na kuyahafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza leo ili tupate matokeo kwenye mchezo ujao hilo pekee litatusaidia kwa sababu ni wazi hatuko kwenye nafasi nzuri katika msimamo wa ligi” alisema.