Friday, 23 October 2015

BAYERN MUNICH WAWANIA USHINDI WA 1,000 TANGU KUANZISHWA KWA BUNDESLIGA KESHO

 

TIMU ya Bayern Munich inaweza kushinda mechi ya 1000 katika Ligi Kuu ya Ujerumani, Bundesliga itakapomenyana na FC Cologne kesho nyumbani, vinara hao wa ligi hiyo wakijaribu kuzinduka kutoka kwenye kipigo cha Arsenal.
Timu ya Pep Guardiola ilifungwa mechi ya kwanza baada ya mechi 13 msimu huu, walipochapwa 2-0 Uwanja wa Emirates Jumanne katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Licha ya kipigo hicho, Bayern bado wapo kileleni mwa Kundi F Ulaya na watakuwa wenyeji wa Cologne Uwanja wa Allianz Arena, wakitoka kushinda mechi zote tisa za Bundesliga hadi sasa msimu huu – na wanakimbilia rekodi mpya ya kushinda mechi ya 10 mfululizo ya ligi.
Ushindi wa 1-0 wiki iliyopita dhidi ya Werder Bremen ulikuwa wa 999 kwa Bayern tangu kuanzishwa kwa Bundesliga mwaka 1963 na The Bavarians wanataka kuzinduka baada ya kuangukia London.
“Hiyo ni Ligi ya Mabingwa. Na kwenye Ligi ya Mabingwa unapaswa kuwa kamili. Hatukuwa,”amesema Guardiola baada ya kipigo cha Arsenal.

Lakini Mwenyekiti wa Bayern, Karl-Heinz Rummenigge ana mtazamo tofauti. “Kwa hakika hakuna cha ajabu kilichotokea. Bado tupo juu katika msimamo," amesema.
“Ni muhimu wachezaji walionyesha kurudi katika mstari sahihi mara moja na kuendeleza wimbi la ushindi. Nataka muendeleze (wimbi la ushindi) dhidi ya Cologne, itakuwa rekodi ambayo itasimama kwa muda wote,”.
Guardiola ana matumaini ya kuwa na mawinga Douglas Costa, Kingsley Coman na Arjen Robben katika mechi na Cologne kesho.

Costa alicheza dhidi ya Arsenal, Coman alikuwa benchi kwa sababu ya majeruhi na Robben anajiandaa kurudi uwanjani baada ya kupona maumivu ya nyonga na amekuwa akifanya mazoezi na wachezaji wa akiba tangu mwanzoni mwa wiki.

0 comments: