Monday, 11 April 2016

Wafanyakazi 597 wa NIDA Walioachishwa Kazi Kuanza Kulipwa Kesho



Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa nchini (Nida) imesema itaanza kufanya malipo ya madai ya wafanyakazi wake 597 waliokatishwa mkataba na mamlaka hiyo hivi karibuni.

Taarifa iliyotolewa jana na Kaimu Mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Modestus Kipilimba, ilisema malipo hayo yataanza kulipwa kesho asubuhi kwenye ofisi za mamlaka hiyo zilizopo katika jengo la BMTL.

Malipo hayo yatafanywa kwa mgawanyo. Mgawanyo wa kwanza utakuwa na kundi la kwanza, pili na tatu, ambao watalipwa kesho na mgawanyo wa pili, utakuwa na kundi la nne na tano ambao watalipwa keshokutwa.

Mgawanyo wa tatu utakuwa na kundi la sita litakalo lipwa Alhamisi, mgawanyo wa nne utahusisha kundi la 7 na 8 litakalolipwa Aprilu 16 na kundi la tano litajumuisha madereva na kada nyingine, litalipwa Aprili 17.

Aidha, taarifa hiyo iliwataka wadai hao kufika kwa wakati sambamba na kuwa na vielelezo na nakala halisi za mikataba yao ya kazi.

Awali, kulikuwa na malalamiko kutoka kwa wafanyakazi hao walioandamana baada ya tangazo la kufutwa kazi kuwa malipo yanayotarajiwa kutolewa na Nida hayasadifu uhalisia wa kile wanachokidai.

0 comments: