Tuesday 12 April 2016

CAGYabainika Madudu Kibao Katika Uhakiki wa Madeni ya Watumishi Wanayoidai Serikali


Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa, Kassim Majaliwa amesema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) , amefanya uhakiki wa madeni yanayodaiwa serikali na watumishi na kubaini madudu kibao.

Amesema madai mengine yameonyesha mashaka ambapo amewataka wakurugenzi wa Halmashauri na Wakaguzi wakuu wa ndani kujiridhisha ukweli wa madai hayo kabla ya kuyafikisha serikalini kwa ajili ya malipo.

“Madai mengine yanatia mashaka, sisi hatuhitaji kuletewa madeni ya hovyo hovyo ni vema Wakurugenzi wa Halmashauri na Wakaguzi wa ndani wakajiridhisha kabla kuyapeleka serikalini kwa ajili ya malipo.

"Madeni mengine ya ajabu, mfano unakuta mtumishi mmoja anaidai serikali sh. milioni 30,  jambo ambalo ni gumu hata kama alihamishwa haiwezekani kufikia kiwango hicho, pia kuna baadhi ya majina yamejirudia mara nne,” amesema.

Waziri Mkuu, Majaliwa ameyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa hospitali ya wilaya ya Ruangwa alipotembelea Hospitali hiyo wakati akiwa katika ziara ya kikazi iliyolenga kukabidhi msaada wa vifaa tiba alivyovitoa kwa ajili ya hospitali hiyo.

Amesema kuwa serikali italipa madeni yote inayodaiwa baada ya kumaliza kuyafanyia uhakiki, hivyo aliwaomba watumishi kuwa na subira wakati serikali ikiendelea zoezi la kuyahakiki ili kuweza kulipa deni sahihi inalodaiwa.

Awali akisoma taarifa ya Idara ya afya kwa Waziri Mkuu, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Dk. Japhet Simeo amesema idara ya afya inakabiliwa na madeni ya watumishi ambayo ni sh. milioni 109,662,483.

Amesema madeni hayo yametokana na likizo, matibabu, uhamisho wa ndani na nje ya wilaya, gharama za mizigo kwa watumishi waliostaafu, ambapo  halmashauri imejipangia utaratibu wa kulipa madeni hayo pindi inapotokea fedha kutoka serikali kuu.

Hata hivyo kasi ya mtiririko wa fedha ni ndogo ukilinganisha na mahitaji halisi ya maslahi ya watumishi ambapo Halmashauri inawapongeza na kuwapongeza watumishi wa Idara ya afya kwa kuendelea kuwa wavumilivu na kuwahudumia wananchi.

Dk. Simeo amesema halmashauri inawapongeza Rais Dk. John Magufuli na Waziri Mkuu, Majaliwa kwa juhudi kubwa wanazozifanya kuongeza mapato nchini, ambapo wana matumaini kuwa watumishi wataboreshewa maslahi na stahiki zao ili kuchochea motisha kiutendaji.

Katika hatua nyingine Dk. Simeo alizungumzia upatikanaji wa dawa, alisema ambao  umeongezeka kutoka asilimia 30 mwaka jana na kufikia asilimia 80 mwaka huu dawa muhimu katika vituo vyote vya kutolea huduma ambavyo viko 32.

0 comments: