Saturday, 9 April 2016

CAG Aikana Ripoti Feki ya NSSF Asema Ripoti itatolewa na Bunge April 25

OFISI ya Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imekana taarifa inayosambazwa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya jamii kuonyesha kuna ufisadi mkubwa kwenye miradi mbalimbali ya Shirika la Taifa la Hifadhi za Jamii (NSSF).

Taarifa ya kuaminika iliyopatikana ndani ya ofisi hiyo na mmoja wa viongozi wa ofisi hiyo, wameeleza kuwa taarifa kamili kuhusiana na NSSF itatolewa na bunge April 25, mwaka huu na wanashangazwa na mambo yanayoenezwa kwenye vyombo vya habari.

Kiongozi huyo mwandamizi huku akikataa kutajwa jina lake alisema hata magazeti hayo yanayoandika uvumi huo, hakuna hata moja linaloeleza kwa ufasaha kuhusiana na ripoti ya CAG.
Ilisema watanzania wanapaswa kutulia na kusubiri taarifa rasmi itakayopelekwa bungeni, kwa kuwa imeeleza kila kitu na sio hicho ambacho kinaonekana kama kinakolezwa na watu wenye maslahi nayo.
"Hata sisi tunashangazwa kumekuwa na msukumo mkubwa na hatujui dhamira yake ni nini, ila tunachoamini tusubiri tu taarifa rasmi ya ripoti itakayopelekwa bungeni,''alisema mtoa taarifa wetu.
Akizungumza na Wabunge wajumbe wa Kamati za Bunge za usimamizi wa fedha, LAAC na PAC, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Profesa Mussa Assad kwenye semina ya mafunzo aliwaeleza wabunge kuwa Ripoti ya CAG anayo yeye na Rais Magufuli tu na anashangazwa na wanaosambaza kinachoitwa taarifa ya CAG wanapata wapi nguvu ya kufanya hivyo.

Profesa Assad alikuwa anajibu maswali ya wabunge ambapo mmoja wa Wabunge kutoka Kambi ya Upinzani alitaka maelezo ya CAG kuhusu kinachoitwa ufisadi katika NSSF.

“taratibu za ukaguzi zinajulikana. Baada ya mkaguzi kuandaa taarifa ya awali hutoa kwa mkaguliwa kujibu hoja za ukaguzi. Kisha Mkaguzi huweza kuziondoa hoja zenye majibu aliyoridhika nayo na baada ya hapo huitwa kikao kinachoitwa ‘exit meeting’ na kukubaliana masuala ya ukaguzi”, alifafanua.

Profesa Assad kwa wabunge wajumbe wa PAC,LAAC na Kamati ya Bajeti. Aliwaeleza wabunge kuwa inawezekana kinachosambazwa ni taarifa ya awali kwa malengo mahususi ambayo yeye kama CAG hawezi kuyajua na kuwataka wabunge wasubiri taarifa yake rasmi itakayowasilishwa Bungeni kabla ya tarehe 25 Aprili 2016.

Kumekuwepo na taarifa mbalimbali, ambazo nyingi zinaonekana zinamtuhumu aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhan Dau aliyeliendesha shirika hilo kwa mafanikio makubwa kuhusishwa na vitendo vya ufisadi wa miradi mbalimbali.

Baadhi ya wachunguzi wa mambo wanasema nguvu inayosukumwa kuichafua NSSF ina lengo la kufifisha nyota ya aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo kabla ya uzinduzi wa daraja la Kigamboni mnamo tarehe 16 Aprili 2016.

0 comments: