Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam,
Mchezaji ambaye amecheza timu ya
Taifa wa miaka 12 mfululizo huku akichezea klabu moja tu maishani na
kubeba majukumu ya unahodha klabuni na timu ya Taifa anaweza kushindwa
kuwa kocha bora mwenye mafanikio endapo tuhuma za kuomba pesa kwa
wachezaji ili awapange katika mechi zitafika mbali na kuainika ni za
kweli.
Kila kitu kina madhara Fulani kwa
kitu kingine, mathalani ‘ Nondo ni mharibu wa vitambaa au nguo za
manyoya, na Kutu hula chuma kigumu bila shida yo yote’. Kuna wakati
akili zetu wanadamu huwa kamili na wakati mwingine huwa si nzima-huwa
leguvu kwa kujiendesha. Hivyo basi, ‘ Sumu ya Mtu ni Kijicho na Chuki’
Chuki ina madhara na kijicho kina aibu kubwa kuliko kitu chochote
ambacho si halali kwa fikra au kwa tendo la kushawishi mtu kula kitu
hicho hata kama kina ‘ ladha’ nyingi kinywani.
Kiungo mshambulizi wa Mtibwa Sugar ( Jina linahifadhiwa kwa
sasa) amesema kuwa kuvurunda kwa timu hiyo msimu huu ni sababu ya kocha
mkuu wa timu hiyo, Mecky Mexime. Mchezaji huyo anayejiandaa kuachana na
timu hiyo mara baada ya kumalizika kwa msimu ameweka wazi kuwa Mecky (
mchezaji –nahodha wa zamani wa timu hiyo na timu ya Taifa, Taifa Stars)
amekuwa akiwapanga timu yake kwa sababu zisizo za kimpira- Kifupi ni
lazima umpatie pesa ili upate nafasi ya kucheza Mtibwa Sugar.
“ Tatizo la Mtibwa ni kocha (
Mecky), ukitoa sababu nyingine, mwalimu huyo amekuwa akipanga timu yake
kama mchezaji utampatia pesa” anasema mchezaji huyo alijiunga na Mtibwa
mwaka 2011 wakati timu hiyo ikinolewa na Mkenya, Tom Olaba. Kwanza
niseme wazi kuwa Mecky ni mchezaji wa zamani ambaye Taifa linamchukulia
kama mfano wa kuigwa kutokana na mchango wake mkubwa alioutoa wakati
alipokuwa mchezaji wa Stars kwa miaka 12 mfululizo.
Nyakati za mwisho za uchezaji
wake, Mecky alijiingiza katika mafunzo ya ukocha huku akiichezea klabu
yake ya Mtibwa na mara baada ya kustaafu soka la ushindani miaka mitatu
iliyopita Mecky alipewa kazi ya ukocha msaidizi katika klabu hiyo
aliyoichezea kwa maisha yake yote na kushinda mara mbili ubingwa wa ligi
kuu, 1999 na 2000. Wakati akiwa msaidizi wa Olaba, Mecky alisimamishwa
na uongozi wa klabu hiyo baada ya kundi kubwa la wachezaji kwenda kwa
utawala wa juu na kulalamikia kitendo cha Mecky kuwashawishi wachezaji
kucheza chini ya kiwango ili timu ifanye vibaya na kocha mkuu Olaba
aonekane hafai.
Mecky alihitaji haraka nafasi ya
ukocha mkuu pale Mtibwa Sugar, akiamini kuwa uzoefu na mbinu za
ufundishaji alizowahi kupata kutoka kwa walimi John Simkoko, Mshindo
Msolla, Burkard Pape, James Siang’a, Salum Mayanga, Olaba, Marcio
Maximo, Jan Poulsen zingeweza kumpatia mafanikio ya haraka. Mtibwa
ilimuajiri Mecky kama kocha mkuu mara baada ya kumalizika kwa mkataba wa
Olaba msimu wa 2011/12 na timu hiyo iliporomoka hadi nafasi ya Tano
ikimaliza nyuma ya Simba SC waliotwaa ubingwa, Azam FC waliomaliza
nafasi ya pili na Yanga SC na Kagera Sugar ambazo zilikamilisha orodha
ya timu nne za juu.
Yalikuwa ni matokeo mabaya zaidi
kwa Mtibwa katika kipindi cha ‘ Muongo Mmoja’ lakini imani kwa Mecky
ilikuwa kubwa kwa kuwa aliingia klabuni na mtazamo wa kuijenga upya
Mtibwa ikitumia zaidi wachezaji vijana kutoka timu ya pili na si
kusajili wachezaji wengi wanaotemwa katika klabu za Yanga na Simba.
Lakini mpango kama huo unahitaji muda zaidi, bila shaka klabu na Mecky
mwenyewe walikuwa wakitambua hilo ndiyo maana wameendelea kufanya kazi
pamoja licha ya timu hiyo kuporomoka hadi nafasi ya Tisa msimu uliopita.
“ Ili kocha akupe namba ni
lazima umpe kocha pesa, hafanyi kwangu tu ni wachezaji wengi wanakutana
na hali hiyo” anaendelea kusema mchezaji huyo ambaye alifanya vizuri mno
msimu uliopita licha ya timu kumaliza katika nafasi mbaya tangu
ilipopanda daraja mwaka 1997. Mtibwa itacheza na Kagera Sugar katika
uwanja wa Kambarage, Shinyanga Jumatano hii wapo nafasi ya nane katika
msimamo baada ya kucheza michezo 18 na kukusanya alama 23 ilianza vizuri
msimu huu na kuongoza ligi kwa miezi mitatu mfululizo lakini
wamefanikiwa kushinda mara moja tu tangu kuanza kwa mwaka huu na sababu
kubwa wachezaji wanasema ni Mecky. Naendelea kumtafuta mwalimu huyo na
chochote atakachosema nitawajuza .
0714 08 43 08
0 comments:
Post a Comment