*Wapambe wasema
alisurubiwa kwa ajili ya urais
NA GORDON
KALULUNGA, MBEYA
WAKATI joto
la urais likizidi kupanda ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana na hofu
ya baadhi ya majina mazito ya wagombea wa nafasi hiyo kuendelea kujitokeza ikiwa
ni pamoja na kujinadi kwa siri, Prof. Sospeter Muhongo, naye amejitosa Katika
nafasi kinyang’anyiro hicho, imefahamika.
Kwa mkoa wa
Mbeya, tayari baadhi ya wapambe wake
wameanza kazi katika wilaya za Momba, Mbeya Vijijini na Mbeya Mjini huku baadhi
ya viongozi wa wanafunzi wa vyuo na vyuo vikuu na waliokuwa katika ngome ya
kundi la Edward Lowassa, wanaongoza kazi ya kumnadi kwa wananchi Prof. Muhongo.
Viongozi hao
baadhi wameelezwa kuwa walikuwa katika kundi la Vijana wa 4U Movement,
linalojinasibu kuwa ni marafiki wa Lowassa.
Mmoja wa
wasomi ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema kuwa ameamua kuondoka katika
kundi la Lowassa kwasababu mbalimbali ikiwemo kundi hilo kuthamini baadhi ya
watu huku wengine hasa wanaofanya kazi kubwa badala ya utapeli kutothaminiwa.
“Hivi
karibuni unakumbuka kuwa kulikuwa na kongamano la Vijana wa 4U Movement hapa
Mbeya, ni kundi ambalo limeamua kujitafutia fedha kwa migongo ya wengine, jambo
ambalo mimi lilinisikitisha na nikaamua kuwaambia hata wakubwa lakini
tunapuuzwa” alisema kijana huyo.
Alipoulizwa kuhusu
yeye pamoja na wenzake kuamua kumnadai Prof. Muhongo wakati hivi karibuni
alijiuzuru kutokana na kashfa ya Escrow, alisema kuwa suala lile mwanasheria
Mkuu alisema Bungeni kuwa yeye ndiye anastahili kubeba lawama lakini
hakusikilizwa baada ya kubaini kuwa Prof. Muhongo hatakuwa anashikika kwenye
Urais hivyo wakaamua kumsulubu baadhi hata bila kujua.
Katika moja
ya kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Nsungwe Hotel juzi mjini Mbalizi wilaya
ya Mbeya Vijijini kati ya wapambe wa kiongozi huyo na vijana wa Bodaboda,
vijana hao walielezwa kuwa ni vema wakaanza kuwa na mtazamo chanya wa kumsema
vema kiongozi mwenye uaminifu, uadilifu, uzalendo na kuona anataka kutupeleka
wapi.
Katika kikao
cha wasomi wa vyuo vikuu na wanataaluma kilichofanyika jana katika bustani ya
City Pub Jijini Mbeya, wasomi hao wamekubaliana kutompoteza kiongozi huyo huku
baadhi wakisifia juhudi zake za kuaminiwa na moja ya Vyuo Vikuu bora kabisa
nchini China, The China University of Geosciences (Wuhan), ambacho kwa
ushawishi wake kimetoa ufadhili wa masomo katika fani ya Mafuta na Gesi (Oil
and Gas Studies) kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili na Shahada ya Uzamivu.
“Jumla ya
nafasi 22 zitatolewa mwaka huu kwa Watanzania watakaokidhi vigezo, ambapo
watapata ufadhili wa masomo hayo kwa asilimia 100 ikiwemo chakula, malazi na gharama
za masomo (tuition fee)” alisema mmoja wa kiongozi wa wapambe wa kiongozi huyo
mkoani Mbeya.
Prof.
Muhongo alipopigiwa simu na mwandish wa habari hizi ili kuthibitisha kama
atawania nafasi hiyo ya urais mwaka huu, alisema kuwa, anafahamu taratibu za
chama chake hivyo hawezi kukubali au kukataa.
“Mimi
nafahamu na kuheshimu taratibu za chama, ukifika wakati chama kikiruhusu kusema
nitasema kama nitawania ama la, lakini niseme kuwa ni wakati sasa wa kumpata
kiongozi anayeaminika na mwenye uwezo wa kujenga uchumi imara unaotoa fursa kwa
kila Mtanzania” alisema Prof. Muhongo.
Aidha alisema
yeye amebahatika kukaa karibu na Mwalimu Julius Nyerere na alibahatika kuambiwa
nini alikuwa anakusudia kuipeleka Tanzania kwa ajili ya Tanzania itakayoendana
na wakati na rasilimali za nchi kuwa tunu kamili za watanzania na siyo kuwa
laana.
0 comments:
Post a Comment