Kiungo mshambuliaji wa City, Peter Samson Mwalyanzi, amesema hesabu zilizopo kwenye kikosi chao hivi sasa ni kushinda michezo yote mitatu ijayo watacheza ugenini dhidi ya Ndanda FC, Azam FC na Yanga SC.
“City itakuwa nje ya Mbeya kwa michezo mitatu, dhidi ya Ndanda, Azam na Yanga, tumejiandaa vyema kuhakikisha tunapata matokeo kwenye michezo yote mitatu, watu wengi wanaweza wasiamini hili ninalosema, lakini kwenye soka inawezekana, tunafahamu jinsi timu hizi zote zinavyocheza kwa kuwa tayari tushakutana nazo. Nina imani tutafanikiwa kushinda zote tatu,” amesema.
Mwalyanzi aliyefanikiwa kurudisha makali yake uwanjani baada ya kusota benchi kwa muda mrefu kufuatia majeraha aliyokuwa nayo, ameweka wazi kuwa kwa sasa City iko kwenye kiwango kizuri tofauti na ilivyokuwa mwanzo, na kwamba hiyo ndiyo jambo pekee inayompa imani ya kufanya kweli kwa kuzikusanya pointi zote tisa dhidi ya timu hizo tatu. “Michezo kadhaa iliyopita tulicheza tukiwa chini ya kiwango na hii ni kwa sababu wachezaji wengi ndani ya kikosi walikuwa majeruhi, kwa sasa ni tofauti kabisa, wote tuko safi na kila mmoja ana ari kubwa ya kucheza kwa mafanikio ili kupunguza kile kilichopotea mwanzoni mwa msimu ndiyo maana nikasema tunataka kushinda mechi zote tatu za nje,” ametamba mchezaji huyo.
Hata hivyo, City itakuwa na mtihani mgumu kupata ushindi dhidi ya Yanga SC ambayo haijawahi kufunga na timu nyingine yoyote ya Ligi Kuu kwenye Uwanja wa Taifa mbali na Simba SC na Azam FC tangu uwanja huo ulipoanza kutumika rasmi 2007.
City haijawahi kuzifunga Azam FC na Yanga SC tangu ipande Ligi Kuu msimu uliopita na timu hizo kwa sasa ndizo zinakimbizana kuwania ubingwa wa msimu huu.
Kikosi cha kocha bora wa msimu uliopita, Juma Mwambusi cha City, kiko nafasi ya 9 katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 23, mbili mbele ya timu iliyoko nafasi ya pili kutoka mkiani mwa msimamo, Polisi Moro FC, hivyo kuwa hatarini kuporomoka daraja.
0 comments:
Post a Comment