Kikao
cha Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania
kilichoketi jumanne ya tarehe 24, Machi 2015 jijini Dar es salaam,
kimepitia taarifa mbalimbali za michezo iliyochezwa na kutoa adhabu kwa
wachezaji na vilabu vya Ligi Kuu ya Vodacom.
Katika mechi namba 107
iliyowakutanisha wenyeji Ndanda FC dhidi ya Coastal Unioni, klabu ya
Ndanda imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa mujibu wa Kanuni ya
42(1) ya Ligi Kuu ya Vodacom kutokana na washabiki wake kumrushia
chupa za maji mwamuzi msaidizi Anold Bugado.
Mechi namba 108 iliyochezwa
Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, (Stand United dhidi Simba SC),
wenyeji timu ya Stand United imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu)
kwa mujibu wa Kanuni ya 14(8) kutokana na timu yake kuchelewa kufika
uwanjani kwa dakika ishirini.
Mchezo namba 117 uliozikutanisha
Simba SC dhidi ya Yanga SC kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam,
timu ya Simba imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa mujibu wa
Kanuni ya 14(9) kwa kukataa kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.
Nayo klabu ya Yanga imepigwa
faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa mujibu wa Kanuni ya 42(11) baada ya
timu yake kuonyeshwa kadi zaidi ya tano kwenye mchezo dhidi ya Simba
SC, huku mshambualiji wake Dany Mrwanda akipigwa faini ya sh. 500,000
(laki tano) kwa mujibu wa Kanuni ya 14(12) kwa kutopeana mikono na
wachezaji wa timu hiyo.
Mchezaji Haruna Niyonzima wa
Yanga amepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa mujibu wa Kanuni ya
37(f) kwa kupiga teke meza ya mwamuzi wa akiba baada ya kutolewa nje
kwa kadi nyekundu. Suala la mshambuliaji wa Yanga Amissi Tambwe kumshika
korodani beki wa Simba SC Murshid Juuko limepelekwa kwenye Kamati ya
Nidhamu.
Kipa wa timu ya Simba SC, Ivo
Mapunda amepewa onyo kwa kufunika tangazo la mdhamini wa Ligi Kuu
(Vodacom) kwa kutumia taulo lake wakati wa mechi dhidi ya Yanga, hatua
kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake iwapo atarudia kufanya tukio
la aina hiyo.
Nao wachezaji Salum Abubakar wa
Azam FC na Richard Maranya wa JKT Ruvu wamepigwa faini ya sh. 500,000
(laki tano) kila mmoja na kusimamishwa mechi tatu kwa mujibu wa Kanuni
ya 37(3) kwa kupigana uwanjani kwenye mechi namba 123 ambapo walitolewa
nje kwa kadi nyekundu.
Klabu ya Kagera Sugar imepigwa
faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa mujibu wa Kanuni ya 14(9) baada ya
timu yake kugoma kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kwenye
mchezo namba 130 dhidi ya Young Africans uliofanyika kwenye Uwanja wa
Taifa.
Mechi namba 132 iliyozikutanisha
Azam na Ndanda SC kwenye uwanja wa Chamazi, klabu ya Ndanda imepigwa
faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) baada ya
washabiki wake kuwamwagia maji na kuwarushia chupa za maji washabiki wa
Azam.
Aidha klabu ya Stand United
imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa mujibu wa Kanuni ya 14(8)
kwa kuchelewa kufika uwanjani kwenye mechi namba 134 dhidi ya timu ya
Mbeya City, pia imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa mujibu wa
Kanuni ya 14(9) kwa kutoingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kwenye
mchezo huo.
Kiongozi wa Stand United, Muhibu
Kanu amepelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu baada ya kuondolewa kwenye
benchi na mwamuzi wa mchezo dhidi ya Mbeya City kutokana na kutumia
lugha ya kuhamasisha vurugu kwa timu yake na kupinga uamuzi wa refarii.
Katika mchezo namba 135
uliochezwa jijini Tanga na kuwakutanisha wenyeji Mgambo Shooting dhidi
ya Yanga SC, Yanga SC imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa
mujibu wa Kanuni ya 42(1) kutokana na washabiki wake kuvamia uwanja
baada ya mechi namba 135 dhidi ya Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa
Mkwakwani.