Friday, 5 September 2014

ASKARI WAFANYIA KAZI NJE MASAA 24, OFFISI KUWA NA NYUFA ZA HATARI,


Jengo la Kituo cha Polisi wilaya ya maswa Mkoani Simiyu , likiwa na nyufa mbalimbali zinazohatarisha kuanguka kwa jengo hilo, huku askari pamoja na mahabusu maisha yao kuwekwa rehani.


Katika hali isiyokuwa ya kawaida kituo cha polisi Wilayani Maswa Mkoani Simiyu kilichopo mjini Maswa  kinakabiliwa na uhaba wa ofisi, ambapo ofisi inayotumika kwa sasa ikihatarisha maisha ya askari na mahabusu.

Jengo hilo ambalo lina vyumba 3 likitegemewa na askari 59 wakiwemo wa upelelezi limejaa nyufa kubwa, ambalo ilielezwa kuwa wakati wowote linaweza kuanguka na kuhatarisha maisha ya watumiaji hao.

Wakiongea na waandishi wa habari kwa masharti ya kutotajwa majina yao askari waliokutwa nje wakiwahudumia wananchi kwa kusikiliza kesi zao, wameeleza kuwa wamekuwa wakipeana zamu kuingia ofisini.

Wamesema kuwa uhaba wa vyumba pamoja na kuhofia kuangukiwa na jengo, imekuwa chanzo cha wao kufanyia kazi nje kwa muda wa saa 24 hali waliyosema inawapa wakati mgumu kufanya kazi.

Wakiongea huku wakionyesha nyufa za jengo hilo ambazo zimeanzia chini hadi kwenye paa, askari hao wamebanisha kuwa  tangu waletwe katika kituo hicho, wamekuwa wakiangaika kutekeleza kazi zao kwa kukosa ofisi za kudumu.

Wamebainisha kuwa mbali na kuangaika kufanya kazi katika mazingira magumu, walisema hakuna mipango yeyote iliyopo ndani ya wilaya pamoja na mkoa ya kujenga kituo kipya cha wilaya cha kisasa chenye hadhi ya Wilaya.

“Hapa nje tulipo ndio ofisi yetu kila siku..wananchi tunawasiliza tukiwa hapa..tunakosa hata meza za kuandikia..ofisi ina vyumba 3 hapa askari tupo wengi sana..wengine tunapeana zamu akimaliza mmoja ofisini anatoka anakuja kukaa hapa nje na mwingine anaingia kusikiliza kesi” Wamesema askari hao.

Hata hivyo imebainika kuwa tangu kuanzishwa kwa wilaya hiyo hakuna jitihada zozote zilizofanywa na jeshi la polisi kujenga kituo cha polisi cha wilaya, ambapo jengo hilo linalotumika jeshi hilo limepanga.

Mbali na kupanga  askari hao wanaeleza kuwepo kwa hatari kubwa ya jengo hilo kuparamiwa na magari (kupata ajali) kutokana kuwa ndani ya barabara kuu ya Simiyu – Shinyanga, huku vumbi linatokana na magari kupita katika eneo hili likihatarisha afya zao.

Mbali na vumbi askari hao wamelalamikia kuwepo kwa kelele kubwa za magari hayo kuwa usumbufu kwao, wakati wanapowahudumia wananchi kwa kukosa utulivu.

Mkuu wa polisi Wilayani Maswa OCD George Salala amekiri kuwepo kwa hali hiyo, huku akibainisha kuwa ofisi yake haina taarifa za kuwepo kwa ujenzi wa ofisi mpya ya Wilaya.

Amesema amepewa taarifa ya kubomolewa kwa ofisi hiyo na TANRODS kutokana na kuwa ndani ya hifadhi ya barabara, hali aliyosema baada ya kubomolewa kwa ofisi hiyo hawana jengo mbadala la kufanyia kazi.

“Ni kweli tunafanyia kazi katika mazingira magumu..kwa muda mrefu hatuna ofisi..ila ilo jengo tunalolitumia kwa sasa limepigwa x (alama ya kubomolewa) sasa baada ya kubomolewa sijui itakuwaje..hatuna ofisi nyingine wala hapa ofisini sina mpango wa makao makuu wa kujenga ofisi mpya” Amesema Salala.

Na Samwel Mwanga-Maswa

0 comments: