Tuesday, 16 September 2014

KOCHA AZAM ABWAGA MANYANGA BAADA YA MECHI NA YANGA SC

 KOCHA wa Azam Academy, Vivik Nagul raia wa India, ameacha kazi baada ya kuitumikia klabu kwa miaka mitatu ya mafanikio.

Nagul aliaga rasmi Azam FC baada ya mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga SC Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Azam FC ilifungwa 3-0.
Nagul aliyeanza kazi Azam FC mwaka 2011, ameondoka baada ya kupata Mkataba mzuri zaidi kwao India.
Nagul alikwenda India kumpeleka mchezaji Ismail Gambo ‘Kussi’ kwa matibabu mwezi uliopita na baada ya kurejea mwezi huu, akatoa taarifa ya kuacha kazi.
Ameondoka; Vivik Nagul ameacha kazi Azam Acadrmy na kurejea kwao India

Nagul aliiongoza Azam FC kwa mara ya mwisho katika mchezo wa utangulizi wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam, Academy ikiwafunga watoto wa Yanga mabao 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Nagul atakumbukwa Azam FC kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kuinua vipaji vya wachezaji waliopandishwa timu ya kwanza kama Joseph Kimwaga, Aishi Manula, Kevin Friday, Farid Mussa, Gariel Michael na wengineo.
Aliiwezesha Azam Academy kutwaa mataji kadhaa kama Kombe la Uhai na Rollingtosn pamoja na pia kuwa tegemeo la timu za taifa za vijana nchini kwa wachezaji wengi wanaozalishwa hapo kuchukuliwa timu za kuanzia U17 hadi U20.
Kwa ujumla, Nagul ameifanya Azam Academy kuwa msingi imara wa vipaji si tu kwa klabu hiyo inayomilikiwa na Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake, bali pia na taifa kwa ujumla.       
Nagul pia kuna wakati alikuwa anakaimu ukocha wa timu ya wakubwa na kuiongoza vizuri, inapotokea dharula za makocha wa timu hiyo kuachishwa kazi.
Na Princess Asia, DAR ES SALAAM

0 comments: