Thursday, 18 September 2014

Polisi Anusurika Kuuawa na baada ya kufamaniwa akitaka Kumbaka Mwanafunzi



Mkuu wa kituo cha polisi cha Nyamboge kilichopo katika kata ya Katoma wilayani Geita mkoani Geita amenusurika kuuawa na wananchi wenye  hasira kali  baada ya kukutwa akitaka kufanya mapenzi na mwanafunzi katika chumba anachoishi mwanafunzi huyo(Geto).

Tukio hilo limetokea juzi  Jumapili  majira ya saa tatu usiku ambapo wananchi wakiwa na marungu na mikuki waliweka mtego wa kumnasa mkuu huyo mwenye namba E 2837 Koplo Venance.

Akielezea tukio hilo binti huyo (jina linahifadhiwa)(19) anayesoma kidato cha nne alisema siku ya jumapili mkuu huyo wa kituo alituma maaskari wawili wiki jana wakaenda kumkamata.

"Hata sijui kosa langu,nilikamatwa nikalazimika kwenda na nilipofika alianza kunilazimisha natembea na mwalimu wangu,nilipokataa nilianza kupigwa na kulazimishwa kuandika maelezo",alisema mwanafunzi huyo.

Alisema baada ya kukataa kuandika maelezo alipelekwa rokapu na muda mfupi baadaye  alifuatwa na askari mmoja kati ya wale waliomfuata anapoishi, alianza kuandika maelezo na kumlazimisha kusaini.

Alisema  baada ya kugoma kuandika alipigwa sana na kuamua kusaini kutokana na kutishiwa kufungwa na baada ya kusaini aliitwa na OCS huyo na kumwambia aende nyumbani lakini arudi jioni ana shida naye ya muhimu sana lakini hakurudi kutokana na kuchoka na kipigo alichokipata kituoni hapo.

"Kutokana na mkuu huyo wa kituo kutuhumiwa na mwanafunzi kuwa anamtaka kimapenzi ilibidi awaambie wanafunzi wenzake na wananchi na baada ya hapo wakatengeneza mtego ili wamnase",walisema mashuhuda wa tukio hilo.

"Siku ya jumapili  mkuu huyo wa kituo alikwenda nyumbani kwa mwanafunzi huyo na kuomba wafanye mapenzi kwa kuwa wenzake anaoishi nao hawakuwepo lakini aligoma kufanya hiyo ",walisema mashuhuda wa tukio hilo  na  kuongeza:

"Kutokana na mtego wa wananzengo,muda mfupi   wananchi waliokuwa wamemuona OCS anakwenda kwa binti huyo walifika hapo na kufunga mlango kwa nje na kuanza kupiga mwano".
 
Walisema kufuatia hali hiyo  OCS huyo alivunja mlango na kutoka nje huku  wanachi wakimkamta na kuanza kumpiga lakini aliokolewa na askari  na kufikishwa  katika kituo kikuu cha polisi cha wilaya ya Geita.

Hata hivyo baadhi  ya wanakijiji waliokuwepo kwenye tukio  hilo walisema OCS huyo amekuwa na tabia mbaya sana kwa wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo kwa kuwatongoza na wakikataa anawasingizia kesi au ndugu zao hivyo kuomba serikali kumchukulia hatua kali OCS huyo kwa kitendo hicho kiovu.

Diwani wa kata hiyo Josephat Komanya  alithibitisha  kutokea kwa tukio hilo na kulaani vikali kitendo hicho na kuwaomba wanafunzi wa kata hiyo kuendelea kuwataja viongozi ambao wanawataka kimapenzi kwa nguvu.

0 comments: