Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma linawasaka watu wasiofahamika wanaotuhumiwa kuingia msikitini na kuiba jeneza, Wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma.
Baada ya kuiba jeneza hilo, watu hao wanadaiwa kwenda nyumbani kwa Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Kitanda, wilayani humo, Fidea Mbawala (30) na kuliweka mlangoni, likiwa limesheheni matofali.
Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Mihayo Msikhela, alisema tukio hilo lililotokea juzi, saa 12:00 asubuhi, katika kijiji hicho.
Alisema tukio hilo limesababisha kuwapo utata na kwamba uongozi wa msikiti umedai kuwa tukio hilo ni la aina yake, ambalo halijawahi kutokea.
Alisema tukio hilo liligundulika wakati waumini wa msikiti huo walipokwenda kuswali swala ya alfajiri na kushtuka baada ya kusikia kuwa jeneza hilo limekutwa kwenye mlango wa nyumba ya afisa mtendaji wa kijiji hicho.
Alisema kwa mujibu wa Katibu wa Msikiti huo, Khalifa Ngonyani, tukio hilo limezua mtafaruku mkubwa kwa waumini wa msikiti huo.
Kamanda Msikhela alisema taarifa za awali zinaonyesha kuwa tukio hilo limefanyika baada ya afisa huyo kuwaeleza wananchi wa kijiji chicho kuwa wanatakiwa kuchangia asilimia 75 ya ujenzi wa shule ya kutwa ya sekondari ya Mkomanile.
Alisema ujenzi wa shule hiyo ni utekelezaji wa agizo lililotolewa na Rais Jakaya Kikwete na kwamba, wanakijiji waligoma kutoa michango hiyo kwa madai kwamba, agizo hilo ni la ghafla na kuomba wachangie mwaka 2015, kwani kwa sasa nguvu zao wameelekeza kwenye kilimo.
Msikhela alisema hakuna mtu aliyekamatwa na kuwa polisi wanaendelea na uchunguzi.
via>>Nipashe
0 comments:
Post a Comment