Habari za kuaminika ambazo MTANZANIA imezipata jana kutoka ndani ya kikao cha wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilichokuwa chini ya Uenyekiti wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, zinasema baadhi ya wabunge walimtuhumu Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangwalah (CCM) kuwa amehongwa na Chama Kilele cha Ushirika (APEX), ili apinge hoja ya Serikali kwa nguvu.
Katika kikao hicho, Dk. Kigwangwalah alituhumiwa kuwa ni miongoni mwa watu ambao wamepewa tenda ya kusambaza pembejeo za kilimo cha wakulima wa tumbaku kupitia kampuni yake binafsi.
Kutokana na mjadala huo kuwa moto, wabunge hao walilazimika kutoka na azimio la kuifuta APEX kama njia ya kunusuru kupitishwa kwa muswada huo.
Chanzo cha kuaminika kililiambia MTANZANIA kuwa kutokana na hoja hizo, ikiwemo tuhuma dhidi ya wabunge na mawaziri kuhongwa na wenye makampuni kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kusambaza pembejeo za kilimo, ilimlazimu Pinda kutumia busara ili kumaliza malumbano hayo.
Baada ya mvutano huo, Dk. Kigwangwalah aliomba nafasi ya kujitetea mbele ya Waziri Mkuu.
Alisema hajawahi kuhongwa na wenye makampuni ya watu wanaosambaza mbolea kwa lengo la kuipigia debe APEX.
“Kilikuwa ni kikao moto, maana ziliibuka tuhuma nzito nzito mno kwa baadhi ya wabunge na mawaziri kuhongwa ili kuweza kufuta APEX kwa lengo la kuwabeba wasambazaji wa pembejeo za kilimo kutoka nje ya nchi.
Mbali ya hilo, MTANZANIA iliambiwa kuwa kutokana na ukali waliokuwa nao wabunge wengi wa CCM, kikao hicho kilimpa onyo Mbunge wa Mpanda Vijijini, Moshi Kakoso (CCM), kutokana na tuhuma zake alizozitoa bungeni dhidi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB), Vita Kawawa pamoja na Makamu wake, Said Nkumba.
Viongozi hao wanadaiwa kuidhinisha mamilioni ya fedha dhidi ya Mkurugenzi Mtendaji wake.
Kutokana na tuhuma hizo, MTANZANIA ilimtafuta Dk. Kigwangwalah ili kupata ukweli kuhusu tuhuma zake za kuhongwa kwa madai kuwa amepewa tenda ya kusambaza pembejeo kupitia Mwenyekiti wa APEX, Moshi Kakoso, ambaye pia ni mbunge wa Mpanda Vijijini (CCM). Alisema hatua ya Bunge kupitisha muswada huo wa sheria ipo siku madudu yataibuka na dhambi itawarudia wabunge waliopitisha, huku wakiifuta APEX kwa maslahi yao binafsi na si ya taifa.
“Daima ninachotaka kusema kuwa mimi ni mfanyabiashara, hata kama ni kutajirika sikutajirika kupitia Bunge, ila kwa kipindi kirefu nilikuwa nafanya biashara ya pamba, lakini hili la kampuni yangu kupewa tenda na APEX si kweli na kama wao wana ushahidi waseme ni kampuni gani.
“Niliapa mbele ya Waziri Mkuu na kikao cha wabunge wa CCM kuwa kama yupo mtu mwenye ushahidi mbele yangu na ajitokeze.
“Mbona kuna taarifa za baadhi ya mawaziri na wabunge kuhongwa ili waweze kupitisha muswada huu na kuifuta APEX. Huu ni ukoloni mamboleo, sasa unarejeshwa nchini kwa mlango wa nyuma,” alisema Dk. Kigwangwalah.
Wakati wa kuhitimishwa kwa mjadala huo jusi, wabunge wa CCM walivuana nguo kwa kutoleana siri zao za ndani, huku Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba (CCM), akijibu mapigo kwa kumtuhumu Mwenyekiti wa APEX, Moshi Kakoso, alisababisha ufujaji wa Sh bilioni 16 za wakulima wa tumbaku
chanzoMtanzania
Alhamisi, Septemba 05, 2013
Na Bakari Kimwanga, Dodoma
0 comments:
Post a Comment