Na Saleh Ally
Neema
imeanza kumjaa kiungo wa zamani wa Simba, Mwinyi Kazimoto baada ya kupiga mabao
mawili safi akiwa na timu yake mpya ya Al Markhiya ya Qatar.
Kazimoto
amefanikiwa kufunga mabao mawili katika mechi tano alizoichezea timu hiyo inayoshiriki
daraja la pili nchini Qatar.
Pamoja na
kufunga mabao hayo mawili katika mechi tano za kirafiki alizocheza, Kazimoto
amefanikiwa kupata namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza.
Kocha wa
zamani wa Simba, Hassan Afif aliyemsaidia Kazimoto kujiunga na timu hiyo nchini
Qatar ameliambia Championi Jumatatu kwamba kocha wake kutoka nchini Serbia
amemhakikishia namba katika kikosi cha kwanza.
“Kweli
amefunga mabao mawili katika mechi hizo tano, walikuwa wamekwenda kuweka kambi
nchini Tunisia na sasa wameisharejea hapa Doha tayari kwa ajili ya ligi
itakayoanza wiki mbili zijazo.
“Kweli
Kazimoto ameonyesha uwezo mkubwa sana kwa kweli, mabao aliyofunga ni mazuri.
Kilichomvutia zaidi kocha ni kwamba, katika mechi zote tano hajacheza dakika 90
katika kila mchezo lakini amefanya vizuri.
“Wakati
mwingine alianza au kuingia katika kipindi cha pili, kocha alifanya hivyo kwa
ajili ya kujaribu wachezaji lakini inaonekana kama amejihakikishia namba katika
kikosi cha kwanza na kocha ametaka aendelee na juhudi hizo,” alisema Afif.
Akiyaelezea
mabao ya Kazimoto, Afif alisema: “Sijayaona lakini kocha kaniambia ni mazuri na
moja lilikuwa ni la shuti kali nje ya eneo la kumi na nane. Imemfurahisha
sana.”
Kazimoto
amejiunga na Al Markhiya akitokea Simba ambayo ameichezea kwa misimu miwili,
kabla ya hapo alikuwa kiungo tegemeo wa JKT Ruvu.
0 comments:
Post a Comment