Tuesday, 4 February 2014

SERIKALI YATOA UFAFANUZI WA BEI ZA MASHINE ZA EFD

 
index
Na Eleuteri Mangi-MAELEZO, Mwanza.
SERIKALI imetoa ufafanuzi wa bei za Mashine za Kodi za Kielektroniki (EFDs) kwa wafanyabiashara kurahisisha ulipaji wa kodi na kufanya biashara yenye tija na ubora nchini.
Kauli hiyo ilitolewa na Kamishna wa Kodi za Ndani wa Mamlaka ya Mapato nchini Patrick Kasera alipokuwa akifafanua na kutoa maelekezo ya bei ya mashine hizo kwa nyakati tofauti jijini Mwanza na Musoma akiwa miongoni mwa wajumbe wa msafara wa Naibu Waziri wa Fedha Adam Malima katika mikoa ya kanda ya Ziwa.
Kamishna Kasera alisema kuwa bei ya chini ya sasa ya mashine za EFD ni sh.600,000/= za kitanzania na gharama ya juu ni sh. 690,000/=.ambapo bei hizo zote zinajumuisha gharama usafirishaji.
Bei iliyotolewa na serikali ni tofauti naile ambayo ilikuwa inawapotosha wafanyabiashara mitaani kuwa ni sh. 80,000/= ambayo si sahihi kulingana na bei halali iliyotolewa na serikali.
“Serikali haifanyi biashara ya kuwaumiza, kuwanyanyasa na kuwaonea na hakuna faida yeyote inayopata inapofanya hivyo kwa watu wake” alisema Kasera.
Kamishna Kasera alisema kuwa serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki yanayorahisisha walipa kodi iliwaweze kutunza kumbukumbu za biashara zao kwa usahihi na usalama kwa kutumia kifaa maalumu kinachoitwa “Fiscal Memory” badala ya mfumo wa zamani wa kuandika kwa mkono.
Mashine hizi ni msaada na zina faida kubwa kwa wafanyabiashara wenyewe ambapo zitaasaidia kutunza kumbukumbu zaidi ya miaka mitano kama sheria inavyotaka.
Kwa upande wa serikali, mashine hizi zitasaidia kutumia kodi zilizokusanywa kutoa mahitaji ya kijamii na kiuchumi kwa wakati kwa wananchi wake ambapo itakuwa nia rahisi kupanga uchumi na kukadiria mapato yake kwa wakati na kwa usahihi.
Kamishna Kasera ametoa rai kwa mwananchi yeyote atakayetaja majina ya watu wanaokwepa kulipa kodi kwa manufaa yao wenyewe na umma kwa ujumla ofisi yake itatoa tuzo kwa atakayefanya hivyo.
“Waleteni watu wanaokwepa kulipa kodi ili mtajirike” alisisitiza Kamishna Kasera.
Rai hiyo kwa mujibu wa Kamishna Kasera iliyoitoa nafasi kwa mtu yeyote kutoa taarifa kwa vyombo husika na kwamba mtoa taarifa atazawadiwa kitita cha hadi  sh. Milioni 20 za kitanzania na jina la mtoa taarifa litahifadhiwa.
Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha wafanyabiashara mkoa wa Mara Baltazari Mwita kwa niaba ya wafanyabiashara alimshukuru Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Fedha Adam Mlima na ujumbe wake kuwa tayari kukaa na wafanyabishara kwa takribani zaidi ya masaa manne kuwaelimisha juu ya matumizi sahihi ya mashine za EFD na faida zake.
Mwenyekiti huyo amemwahidi Naibu Waziri Malima kuwa wafanyabiashara wote wapo tayari kufuata elimu waliyopewa katika mkutano huo kwa manufaa yao wenyewe na taifa kwa ujumla.
Naye mfanyabiashara wa jijini Mwanza Leopord Kurugira alisema kuwa wafanyabiashara hawana shida na mashine za EFD, wao wanahitaji kupewa elimu zaidi juu ya mashine hizo.
Zaidi ya hayo Karugura alimshukuru Naibu Waziri na ujumbe wake kuongea nao na kuwapa elimu ya mashine za EFD ambazo mwanzoni wao kama wafanyabiashara hawakupata elimu ya kutosha na kuwasababisha kuziogopa badala ya kuzitumia.
Kamishna Kasera aliifafanua zaidi kwa wafanyabiashara wa mkoani Mara na Mwanza juu ya mashine za EFDs na alisema kuwa mashine hizo kazi yake kuu ni kutunza kumbukumbu za biashara hasa manunuzi na uuzaji wa bidhaa na huduma mbalimbali na sio mfumo wa kodi kama ilivyopokelewa mwanzoni na wafanyabiashara nchini.
Mashine za EFD ambazozinatumika zipo za aina tatu ambazo ni Rejesta za kodi za Kielektroniki (ETR), Printa za Kielektrniki za kodi (EFP) na Mashine za Alama za Kielektroniki za kodi.
Ziara ya Naibu Waziri wa Fedha ililenga kutembelea vituo vya forodha, TRA vya Rusumo, Kyaka, Mtukula na Bukoba mjini katika mkoa wa Kagera, Tarime, Sirari na Musoma mjini katika mkoa wa Mara na jijini Mwanza ambapo pote alipotembelea alizungumza na wafanyabiashara katika mikoa hiyo ya Kanda ya Ziwa.

0 comments: