Friday, 5 September 2014

AGA KHAN YATOA MSAADA WA KWA HOSPITALI ZA HALMASHAURI 4 ZA MBEYA‏


 Mwenyekiti wa kamati ya afya Aga Khan Mbeya (kushoto)Sultan Thawer, akitoa taarifa kabla ya kukabidhi msaada wa vifaa vya tiba kwa Halmashauri nne za Mkoa wa Mbeya.
 Mwenyekiti wa kamati ya afya Aga Khan Mbeya (kushoto)Sultan Thawer, akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro kabla ya kukabidhi msaada wa vifaa vya tiba kwa Halmashauri nne za Mkoa wa Mbeya.


 Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro,akisaidiwa na Mganga mkuu wa Mkoa,Dk. Seif Mhina,Katibu tawala Mkoa wa Mbeya, Mariam Mtunguja na Mwenyekiti wa Kamati ya afya Aga Khan Sultan Thawer wakikata utepe kuashiria kukabidhi msaada wa vifaa hivyo.
 Mwenyekiti wa kamati ya afya Aga Khan Mbeya,Sultan Thawer, akipongezwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro baada ya kukabidhi msaada.
 Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro akiangalia baadhi ya vifaa vilivyotolewa na Hospitali ya Aga Khan.
 Meneja wa Hospitali ya Aga Khan Mbeya, Abel kide, ambaye pia ni mratibu wa Mradi wa tuunganishe mkono pamoja akimuonesha moja ya mashine mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro.
 Mkuu wa Mkoa na viongozi wa Aga Khan wakiangalia moja ya mashine zilizokabidhiwa kwa Halmashauri nne za Mkoa wa Mbeya.
Picha ya pamoja

HOSPITALI ya Aga khan ya Mbeya imetoa msaada wa vifaa tiba kwa Hospitali na vituo vya afya katika Halmashauri nne za Mkoa wa Mbeya vyenye thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 300.
Msaada huo ulikabidhiwa  na uongozi wa Hospitali hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro kwa niaba ya Halmashauri husika katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mkapa uliopo Sokomatola jijini hapa.
Mratibu wa Mradi wa tuunganishe mkono pamoja(JHI) Mkoa wa Mbeya, Abel Kide, ambaye pia ni Meneja wa Hospitali ya Aga Khan alisema Halmashauri zilizonufaika na mradi huo ni pamoja na Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Kyela, Mbozi na Momba.
Kide alizitaja Hospitali na zahanati zinazopatiwa vifaa hivyo kuwa ni Zahanati ya Ngana na Hospitali ya Wilaya ya Kyela(Kyela), Zahanati ya Iyunga na kituo cha Afya Kiwanja Mpaka(Mbeya jiji), Hospitali ya Wilaya ya Mbozi(Vwawa)na Zahanati ya Ivuna iliyopo wilayani Momba.
Alivitaja vifaa hivyo kuwa ni Vitanda vya kujifungulia wajawazito, vitanda vya wagonjwa wa kawaida, Mashine za kuchemshia vifaa vya hospitalini, Mashine ya kumpa joto mtoto aliyetoka kuzaliwa, Mashine ya Ultra Sound,Mashine ya kumtolea uchafu mtoto mchanga,mashine za kupima uzito, joto, urefu na Presha na kwamba vyote jumla vinagharimu zaidi ya shilingi Milioni 300.
Kide alisema lengo la kutoa msaada huo ni kuboresha afya ya mama mjamzito, mtoto mchanga na mtoto aliyechini ya miaka mitano ikiwa ni pamoja na kusogeza huduma za afya  karibu na wananchi hususani kuokoa vifo vinavyotokea wakati wa kujifungua.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbasi Kandoro alipongeza Hospitali ya Aga Khani kwa Msaada waliotoa katika Halmashauri hizo na kuziomba taasisi zingine kuungana na Serikali katika mpango wa kuhakikisha vifo vya Wanawake wajawazito, watoto wachanga na waliochini ya umri wa miaka mitano vinapungua.
Kandoro alisema mkakati wa kupunguza vifo hivyo hautafanikiwa ikiwa utakuwa ukifanywa na sekta moja ya afya pekee bali kwa kushirikisha sekta zingine  binafsi za serikali, viongozi wa dini na vyombo vya habari.
Aliongeza kuwa ili kukomesha kabisa vifo hivyo, Halmashauri zitenge bajeti za kununua mfumo wa huduma tembezi(Mobile clinic) ili ziweze kufika hata maeneo ambayo hakuna huduma ya afya kwa kuwasogezea wananchi huduma ili waweze kupata msaada wa matibabu wakati wowote.
Sambamba na kupokea msaada huo Mkuu wa Mkoa wa Mbeya alizindua Mpango wa utekelezaji wa kupunguza kasi ya vifo vitokanavyo na matatizo ya uzazi, watoto na watoto waliochini ya umri wa miaka mitano.

Kandoro aliongeza kuwa mkakati huo ni maagizo ya Raisi wakati wa uzinduzi wa kitabu cha Mkakati wa kitaifa uliofanyika Mei 15 Mwaka huu ambapo aliagiza Kila Mkuu wa Mkoa kuutafakari mkakati huo kulingana na mazingira wanakotoka.

Na Mbeya yetu Blog

0 comments: