Monday, 10 February 2014

USHINDI WA MTOTO WA DR MGIMWA JIMBO LA KALENGA , WAWAGAWA WANA CCM WASEMA WAPO TAYARI KUKIPUMZISHA CCM HADI 2015


Rais Dr Jakaya  Kikwete akimfariji  mtoto wa Dr Wiliam Mgimwa Bw Godfrey Mgimwa  wakati wa mazishi ya  babake hivi karibuni ,mtoto  huyo  ndie mshindi wa kura za maoni ubunge jimbo la kalenga kupitia CCM.
...................................................................................

IKIWA ni  siku tatu  zimepita  toka wana CCM jimbo la Kalenga  kumchagua kwa  kura za  kishindo  Godfrey Mgimwa ambae ni mtoto  wa aliyekuwa mbunge wa jimbo la Kalenga marehemu Dr Wiliam Mgimwa hali  ya  kisiasa ndani ya  CCM Kalenga si shwari  baada ya ushindi wa mtoto  huyo wa Dr Mgimwa  kuonyesha kuwagawa wananchi na wana CCM.

Uchunguzi  uliofanywa na mtandao huu wa   katika maeneo  mbali mbali ya  jimbo hilo baada ya ushindi huo mkubwa alioupata mtoto wa Dr Mgimwa wengi  wanaonyesha  kuwapinga  wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM ambao  waliamua  kumpigia kura Mgimwa kwa  madai  kwa kufanya hivyo  ni  sawa na  kulitoa sadaka  jimbo hilo kwa vyama  vya upinzani.

Ajuaye Kalinga  alisema  kuwa upinzani  katika  jimbo la Kalenga  haupo kabisa   ila  kutokana na uamuzi mbaya  uliofanywa na  wajumbe  hao  wa CCM kwa kumchangua mrithi wa Dr Mgimwa kuwa ni mtoto  wake  ni  wazi upinzani utaingizwa Kalenga na  wana CCM wenyewe ambao hawaungi mkono uamuzi huo.

Kalinga  alisema ni heri angechaguliwa  mwana CCM mwingine kata ya  wanachama tisa  waliojitokeza kuliko  kumchagua mtoto  wa aliyekuwa mbunge wa jimbo  hilo kwani kwa  kufanya hivyo ni  wazi CCM itapoteza sifa na kuingia katika  wakati mgumu kwa  kuendekeza siasa  za kubebana na siasa za kifamilia.

" Tunashindwa  kujua  wajumbe wa mkutano huo wa  kura za maoni jimbo la Kalenga  walikutwa na nini  hadi kuamua  kutoa kura za rambi rambi kwa  mtoto wa mbunge  Dr Mgimwa ....siku zote  CCM tumekuwa  tukiutumia udhaifu wa Chadema  wa  kukifanya chama hicho kuwa  cha   watu wa Kaskazin kwa maana ya   wachaga   wakati leo CCM tunauonyesha umma  kuwa CCM Kalenga ni mali ya familia ya akina Dr Mgimwa "alisema 

 Kuwa  mbali ya  kuwa  kumkata jina la mtoto  wa  Dr Mgimwa itapelekea  waliomchagua kuchukia uamuzi huo  ila ni  heri kufanya hivyo kwa  kukifanya chama  hicho kuondokana na aibu ya kuwa  chama cha ukoo kuliko kumkumbatia kwa  kumfuta machozi mtoto wa Dr Mgimwa jambo  ambalo ni hatari  ni njia kwa upinzani  kutumia nafasi hiyo  kuuthibitishia umma kuwa CCM ni chama cha familia na viongozi na  watoto  wao.

Hata  hivyo  alisema  kuwa wananchi wa kalenga  ambao ni  wana CCM wasio viongozi  wala  wajumbe  wamepanga  kukutana mara  baada ya uteuzi wa mwisho  wa CCM ili kutoa msimamo  wao   juu ya suala  hilo kama CCM iendelee kuongoza  jimbo  hilo ama  kuelekeza kura zao kwa Chadema .

"Sisi  kama  wana kalenga kweli hatujapendezwa na uamuzi wa  wenzetu  waliokwenda mjini kushiriki  kuchagua ....sasa  wale walikuwa na nafasi  ndani ya  chama ila  sisi tusio na nafasi ya kushiriki kuchagua ndani ya CCM tutatoa uamuzi wetu mgumu na  tunaomba  wajumbe  wote  zaidi ya 800 walioshiriki kura za maoni kura  zao  wampe mtoto wa Mgimwa ila  sisi wananchi zaidi ya 200,000 jimbo la kalenga tunajua  kwa  kupeleka kura  zetu...kwani  kura ni siri  yetu"

Huku Yohana  Sanga  akidai kuwa  kilichotokea jimbo la Arumeru Mashariki   kwa  kumpeleka  bungeni  mgombea wa Chadema  Joshua Nassar ndicho  kitakachotokea katika  jimbo la Kalenga kwa  kuipumzisha  CCM kwa kipindi  hiki kifupi  cha mwaka mmoja na nusu hadi 2015  kwa kumchangua mgombea wa Chadema hata akiwa ni mpiga debe stendi  watampa  kura zao  kuliko  kubariki siasa za kifamilia  katika  jimbo hilo.

"  Tunakipenda sana chama chetu  CCM na ndio sababu ya jimbo la Kalenga  hata upinzani hauna nguvu  ukilinganisha na maeneo mengine  ila katika  hili lazima wana Kalenga tuseme basi yatosha kwa wajumbe wa Halmashauri  kuu ya CCM jimbo  kutuchagulia mgombea ambae ni mtoto  wa marehemu sisi tuna uamuzi  wetu  ila sio kauli  ya kupenda bonga  penda na ua lake....tulipenda bonga Dr Mgimwa  ila Mungu kampenda zaidi yetu  na sio kulazimisha upendo kwa ua lisilo  zaa matunda kwetu  kwani  kuendelea  kumpa kura za rambi rambi mtoto wa Dr Mgimwa ni  sawa na kukaa katika tawi la mti unalolikata mwenyewe "

Alisema  wana  Kalenga  wapo tayari kumpigia kura  mgombea  yeyote wa CCM kati ya  wagombea 9 walioingia katika mnyukano  huo  ila  si mtoto  wa Dr Mgimwa kwani  ubunge  si nafasi  za kurithiana kifamilia na si kweli kuwa ukoo  wa Dr Mgimwa ndio wenye nafasi ya  kuendelea  kuongoza jimbo  hilo .

" Tunajua  kauli mbali mbali za viongozi wakati wa mazishi ikiwemo  ile ya katibu mkuu wa CCM na waziri  mkuu kuwa  wataendelea  kuisaidia familia ya Dr Mgimwa ila kama msaada wenyewe ndio wa  kupeana nafasi za uongozi  wana Kalenga  tunasema msaada huo ni kaa la moto kwa CCM ni  wasije tafuta mchawi baada ya matokeo "

Katika uchaguzi huo wa kura za maoni Mtoto wa Mgimwa alishinda kwa kura 342 huku Jackson Kiswaga akipata kura 170 na mkuu wa wilya ya Pangani Hafsa Mtasiwa akiambulia kura 42 .
Wagombea wengine ni pamoja na  Peter Mtisi akipata kura 33 ,Msafiri Pangagira kura 8,Bryson Kibasa kura 7,Edward Mtakimwa kura 3 na Thomas Mwiluka akiambulia kura 2.

0 comments: