Dar es Salaam. Jumla ya watu 27
wamepoteza maisha yao na wengine 27 wamejeruhiwa katika matukio
yanayohusisha ajali za treni zilizotokea nchini mwaka jana. Kamanda wa
Kikosi cha Reli Tanzania, Saada Haji akizungumza na gazeti hili alisema
kwamba jumla ya ajali 79 zinazohusisha treni zilitokea mwaka jana
katika mikoa tofauti nchini.
Alisema kuwa hata hivyo, ajali nyingi kati ya hizo
zimetokana na uzembe, ikiwemo kulewa na kukaa juu ya reli, kuweka
‘headphone’ na kutembea relini na madereva wa magari kukosa umakini wa
kufuatilia alama za barabarani kwa kuendesha mwendo kasi hata mahali
penye kivuko cha treni.
“Treni linalofanya safari zake ndani ya jiji ndiyo
ambalo kwa sasa linahusisha vifo vya watu wengi kwa muda mfupi tangu
kuanza kwa safari zake watu 8 wamekufa huku wengine wakijeruhiwa,”
alisema Kamanda Haji.
Alisisitiza, ” Hasa katika eneo la Daraja la
Buguruni kwa Mnyamani ndiyo eneo ambalo ni hatari, kwani limekuwa na
matukio ya ajali, wananchi wengi hujisahau hukatiza juu ya reli kwa kuwa
treni huwa halina breki za papo kwa papo basi vifo au majeraha makubwa
yanayowasababishia ulemavu wa kudumu,” alibainisha.
Akizungumzia kuhusu matukio 285 ya uhalifu
alisema kuwa yalitokea katika M ikoa ya Morogoro, Dodoma, Tabora,
Mwanza, Kigoma, Mpanda na Dar es Salaam, ambayo yalitokea katika
maeneo ya reli na ndani ya treli.
“Polisi wa kikosi hiki wamekuwa wakipambana
kikamilifu, kuna siku walifanikiwa kukamata mabegi yaliyowekea bangi,
ambapo mtuhumiwa alifikishwa mahakamani kujibu mashtaka,” alisema.
Alisema kuwa Polisi hao pia waliwahi kumbaini
mhalifu mmoja aliyekuwa amebeba silaha isivyo halali ndani ya treni
ambaye alikurupuka na kuitelekeza silaha hiyo.
Na Beatrice Moses, Mwananchi













0 comments:
Post a Comment