- 16:32 Kura zimeanza kuhesabiwa katika vituo mbalimbali. Kwenye picha hapa chini, kura zinahesabiwa katika kituo cha shule ya upili ya Ben Bella.
16:24 Katika kituo cha shule ya upili ya Ben Bella, shughuli ya upigaji kura imekamilika, masanduku yakafunguliwa na karatasi za kura zikaanza kupangwa tayari kuanza kuhesabiwa.
16:00 Vituo vya kupiga kura sasa vyafaa kufungwa rasmi. Wapiga kura walio vituoni hata hivyo wanaruhusiwa kupiga kura hadi saa kumbi na mbili jioni.
15:50 Vituo vya kupigia kura vinafaa kufungwa saa kumi. Katika kituo cha Madungu, Pemba hakuna wapiga kura waliosalia. Watu pekee ni maafisa wa usalama, maafisa wa tume na mawakala wa vyama.
15:30 Mwandishi wa BBC aliyeko Pemba Arnold Kayanda anasema wakazi wametumiwa ujumbe wa SMS wa kuwasihi wakapige kura.
Ujumbe umekuwa hivi: "Unahimizwa kuja kupiga kura muda huu. Kuna usalama, utulivu na hakuna foleni. Mwambie na mwenzio. Afisa Uchaguzi wa Jimbo."
14:00 Wawafahamu wagombea wote wa urais walio kwenye karatasi za kura visiwani Zanzibar? Kuna wagombea 14. Majina yao ndiyo haya:
1 | Khamis Iddi Lila | ACT-W |
2 | Juma Ali Khatib | ADA-TADEA |
3 | Hamad Rashid Mohamed | ADC |
4 | Said Soud Said | AFP |
5 | Ali Khatib Ali | CCK |
6 | Ali Mohamed Shein | CCM |
7 | Mohammed Massoud Rashid | CHAUMMA |
8 | Seif Sharif Hamad | CUF |
9 | Taibu Mussa Juma | DM |
10 | Abdalla Kombo Khamis | DP |
11 | Kassim Bakar Aly | JAHAZI |
12 | Seif Ali Iddi | NRA |
13 | Issa Mohammed Zonga | SAU |
14 | Hafidh Hassan Suleiman | TLP |
13:00 Mji Mkongwe (Stone Town) ambao ni maarufu sana kwa watalii hauna watu wengi. Mwandishi wa BBC Tulanana Bohela amepiga picha hizi zinazoonesha mtaa huo ukiwa kama mahame.
11:15 Mwandishi wa BBC Halima Nyanza aliyeko Zanzibar anasema idadi ya watu waliojitokeza katika baadhi ya vituo ni ndogo, tofauti na uchaguzi wa awali Oktoba 25, mwaka jana. Baadhi ya mitaa imeonekana kutulia huku ulinzi ukiwa umeimarishwa katika baadhi ya maeneo.
10:30 Mgombea urais wa chama cha ADC Hamad Rashid amepiga kura yake kituo cha Tondooni Wawi wilaya ya Chake-Chake, mkoa wa Kusini Pemba. Amesema: "Nina imani ya kuwa Rais, nikikosa nitakuwa Makamu wa Rais".
10:00 Mwanamke akitumbukiza kura kwenye kijisanduku kituo cha Kiembe, Samaki. Upigaji kura unaendelea.
08:50 Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM) visiwani Zanzibar Dkt Ali Mohammed Shein amezungumza na wanahabari baada ya kupiga kura yake katika kituo cha Bungi, Kibera kisiwani Unguja.
Mwanzo amezungumzia hatua ya Chama cha Wananchi (CUF) kususia uchaguzi huo.
Kuhusu amani na utulivu, amesema anaamini kutakuwa na utulivu visiwani.
08:13 Kumbuka, Chama cha Wananchi (CUF) kilitangaza kwamba hakitashiriki uchaguzi wa marudio unaoendelea leo. Chama hicho kinaamini kilishinda uchaguzi uliofanyika tarehe 25 Oktoba mwaka jana na mgombea wake Maalim Seif Hamad anafaa kutangazwa mshindi.
Tume ya uchaguzi Zanzibar hata hivyo ilitangazwa kwamba hakuna aliyejiondoa rasmi kutoka kwa uchaguzi wa leo.
08:00 Maafisa wa usalama wakishika doria mjini Chake kisiwani Pemba.
07:50 Safari zote za meli kati ya bandari ya Dar es Salaam na visiwa vya Zanzibar zimekatizwa.
Hapa chini ni tangazo la kuwapasha wateja wa Azam Sealink kwamba hakutakuwa na safari za meli kuanzia tarehe 18 hadi 22 Machi kutokana na uchaguzi unaoendelea Zanzibar.
Licha ya kukatizwa kwa safari, badi wapo watu waliojitokeza wakitarajia kusafiri. Wengi wa waliofika ni wageni kutoka Ulaya ambao hawakuwa na habari.
07:44 Usalama umeimarishwa visiwani. Hapa chini ni maafisa wa usalama wakiwa na mbwa wa kunusa kabla ya Dkt Shein kupiga kura yake katika kituo cha Bungi, Unguja.
07:42 Baadhi ya wapiga kura wakitafuta majina yao kituoni Madungu Chake-Chake, kisiwani Pemba.
07:30 Mwanamke akipakwa wino kwenye kidole chake baada ya kupiga kura kituo cha Madungu Chake-Chake, Pemba.
Baadaye, atabasamu baada kutoka nje ya ukumbi.
07:20 Hii hapa ni picha nyingine ya Dkt Ali Shein, mgombea urais wa CCM baada yake kupiga kura Unguja.
07:05 Mgombea wa Chama cha Mapinduzi Dkt Ali Mohammed Shein amepiga kura yake katika kituo cha Bungi, Kibera katika kisiwa cha Unguja.
07:00 Vituo vingi vya kupigia kura vimefunguliwa.
06:50 Maafisa wa uchaguzi wanajiandaa kufungua vituo. Vituo vinafunguliwa saa moja asubuhi na kufungwa saa kumi alasiri.
06:40 Wapiga kura kituo cha Bungi, Unguja wasubiri kituo kifunguliwe.
06:35 Katika vituo vingi, wapiga kura hajawafika. Lakini maafisa wa tume tayari wamo vituoni pamoja na maafisa wa usalama. Hata ni kituo cha Madungu Chake-Chake, Pemba.
06:30 Hujambo! Wapiga kura visiwani Zanzibar wanashiriki uchaguzi wa marudio leo baada ya matokeo ya uchaguzi uliofanyika 25 Oktoba mwaka jana kufutwa na tume ya uchaguzi. Chama cha CUF kinasusia uchaguzi huo.
Karibu kwa taarifa za moja kwa moja kuhusu uchaguzi huo.
0 comments:
Post a Comment