Asifiwe George, Dar es Salaam na Janeth Mushi, Arusha
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wametofautiana katika tarehe ya uchaguzi wa meya na naibu meya wa Jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Simbachawene, alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe, kuitisha uchaguzi huo kabla ya Machi 25, mwaka huu.
Alisema Serikali ina dhamira ya dhati ya kutaka kufanyika kwa uchaguzi huo ili wananchi wapate maendeleo kupitia wawakilishi wao.
Kutokana na sintofahamu ya uchaguzi huo, alisema Serikali inataka ufanyike kwa kufuata misingi ya kisheria na kidemokrasia ili wananchi waanze kupata huduma kupitia vyombo vyao vya uwakilishi.
“Serikali inatoa wito kwa wadau wote wa siasa na kuwataka kukaa na kutafakari wakiwa na nia na dhamira ya kweli ya kutaka uchaguzi huu ufanyike,” alisema Simbachawene na kuongeza:
“Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam aitishe haraka kikao cha uchaguzi huo na kikao hicho kifanyike si zaidi ya Machi 25, mwaka huu kwa kuwa sintofahamu hiyo imechukua muda mrefu.”
Alisema ulishindwa kufanyika kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo utata wa wajumbe wanaostahili kuhudhuria kikao cha uchaguzi huo na Serikali ilichukua hatua mbalimbali ikiwemo kutoa mwongozo wa taratibu za kuitisha na kuendesha mkutano wa kwanza wa Februari 4, mwaka huu.
“Serikali ilimwelekeza Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam na Wakurugenzi wa Halmashauri za Manispaa ya Ilala, Temeke na Kinondoni kuhakikisha wanarekebisha kasoro zilizojitokeza za wajumbe na mamlaka hizo ili ushiriki wao utokane na misingi na maelekezo ya kisheria,” alisema Simbachawene.
Alisema uchaguzi huo ulipangwa kufanyika Februari 8, mwaka huu lakini haukufanyika baada ya wabunge wa viti maalumu na wabunge kutoka Manispaa ya Kinondoni na Ilala kudaiwa kuwa wao si wakazi.
Alisema kutokana na sakata hilo, Serikali iliwaelekeza wakurugenzi wa manispaa hizo kuhakikisha wanawasilisha kwa Kabwe orodha ya wajumbe wanaostahili kupiga kura ili kumchagua meya na naibu meya.
Alisema uchaguzi huo ulipangwa tena kufanyika Februari 27, mwaka huu hata hivyo haukufanyika baada ya halmashauri ya jiji kupokea amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyositisha uchaguzi wa meya hadi shauri la maombi ya uchaguzi (election petition) lililofunguliwa litakaposikilizwa.
Aliwataja walalamikaji katika shauri hilo namba 34/2016 ni Susan Masawe na Saad Khimji dhidi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambayo ilitokana na shauri la uchaguzi (election petition namba 2/2016), hivyo hatua hiyo ilisababisha vurugu na kusababisha baadhi ya maofisa wasimamizi wa uchaguzi kupigwa na kuchaniwa nguo na uchaguzi kuahirishwa.
Pia alisema amri ya kuzuia uchaguzi huo ya Februari 27, mwaka huu imebainika haikuwa halali kutolewa katika kikao hicho cha Februari 27, mwaka huu.
“Hata hivyo, Februari 23, mwaka huu shauri la maombi (election petition) lililokuwa limefunguliwa liliondolewa mahakamani na hivyo kuifanya order hiyo isiwe na uhalali wowote kwa kuwa ilikuwa feki,” alisema Simbachawene.
Baada ya Simbachawene kutoa agizo hilo, Ukawa walitaka uchaguzi huo ufanyike Machi 18, mwaka huu.
Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Madiwani na Wabunge wa Ukawa wa Jiji la Dar es Salaam, John Manase, alitoa msimamo huo jana kwa niaba ya wenzake baada ya kuvamia ofisi ya Kabwe wakitaka watajiwe tarehe ya kufanyika uchaguzi huo ndipo walipoelekezwa kwenda Tamisemi ambako waliambiwa Simbachawene ameshatangaza tarehe ya uchaguzi huo.
Walipokwenda ofisi za Tamisemi walijibiwa na Naibu Katibu Mkuu Tamisemi, Dk. Deo Mtasiwa, kuwa hakuna sababu ya uchaguzi huo kushindwa kufanyika mapema kwa kuwa vikwazo vinavyosababisha uchaguzi huo ushindwe kufanyika vimeisha kwa kuwa mahakama imeshatoa hukumu kuhusu zuio feki.
“Mwanzo uchaguzi uliahirishwa kutokana na kutolewa hati feki na mahakama ya kuzuia uchaguzi usifanyike lakini tayari mahakama imeshatoa hukumu kuhusiana na zuio hilo, hivyo hatuoni sababu ya wao jiji kuendelea kutoa tarehe za mbali wakati wananchi wanataka kumpata meya ili maendeleo ya jiji yaweze kupatikana kwa haraka,” alisema Dk. Mtasiwa.
Baada ya kujibiwa hivyo, Ukawa walimuomba Dk. Mtasiwa awasiliane na Kabwe ili kumshauri uchaguzi ufanyike Machi 18, mwaka huu na itakaposhindikana wataamua cha kufanya.
Katika hatua nyingine, walirudi tena katika ofisi za Kabwe ili kukutana naye wajadiliane tarehe ya uchaguzi lakini hawakumkuta ofisini kwake na kuacha ujumbe kisha wakaahidiwa warudi keshokutwa.
0 comments:
Post a Comment