Idara ya Uhamiaji nchini imefanya mabadiliko ya maofisa waandamizi kwa kuwahamisha vituo vya kazi kuanzia ofisi ya makao makuu, mikoa, wilaya na mpakani.
Pangapangua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga alilolitoa kwenye kikao chake na viongozi wakuu wa idara hiyo kilichofanyika Februari 23.
Siku hiyo, Waziri Kitwanga aliagiza kufanyika kwa mabadiliko hayo kutokana na kukithiri kwa vitendo vya upitishaji dawa za kulevya na wanyama hai kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na Kilimanjaro (KIA) na kwenye mpaka wa Tunduma, Mtukula, Halolili na Kasumulo.
Pia, aliagiza kuhamishwa kwa wakuu wa upelelezi wote wa wilaya za Dar es Salaam na maofisa wa uhamiaji waliokaa kwenye kituo kimoja kwa zaidi ya miaka mitatu, huku akisema huo ni mwanzo wa mabadiliko makubwa kwenye idara hiyo.
Akitangaza mabadiliko hayo jana, Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Abbas Irovya (pichani), alisema upanguaji huo unalenga kuimarisha utendaji, ufanisi na dira katika idara hiyo.
“Pamoja na orodha hii ya maofisa waandamizi wanaohama vituo vyao vya sasa kwenda vituo vingine, Idara ya Uhamiaji inaendelea na utaratibu wa kuwabadilisha vituo vya kazi maofisa zaidi ya 200 kutoka sehemu mbalimbali nchini ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga,” alisema.
Irovya, ambaye alitangaza mabadiliko hayo kwa niaba ya Kaimu Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, alisema amewahamisha Ofisa Uhamiaji, Faustine Nyaki, aliyekuwa mkoani Iringa, kwenda Mwanza kuwa ofisa uhamiaji wa mkoa.
Wengine waliohamishwa ni Remigius Pesambili (Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Mwanza), anayekwenda kuwa mfawidhi wa ofisi ya Uhamiaji ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Rose Mhagama (Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Geita) anayehamia Njombe.
Assa Mwansansu aliyekuwa Mfawidhi wa Kitengo cha Hati za Ukazi, anahamia Pwani kuwa ofisa uhamiaji wa mkoa, Safina Muhindu (Ofisa Uhamiaji wa Wilaya ya Ilala), anahamia Morogoro kuwa ofisa wa mkoa na Wilfred Marwa (Naibu Ofi sa Uhamiaji wa Tanga), anayehamia Geita kuwa ofisa uhamiaji wa mkoa.
Alisema Evarist Mlay (aliyekuwa Ofisa Uhamiaji wa Wilaya ya Kinondoni) anahamia Wilaya ya Same, wakati Frank Mwakifuna (aliyekuwa Ofisa Uhamiaji Same), anahamia Kinondoni, huku Pilly Mdanku (ofisa wa hati za kusafiria wa Makao Makuu), anakuwa Ofisa Uhamiaji wa Wilaya ya Ilala na George Goda (kitengo cha Hati za Ukazi Makao Makuu) anahamia Temeke kuwa ofisa uhamiaji wa wilaya.
Mwingine aliyehamishwa ni jafari Kisesa, ambaye alikuwa ofisa Uhamiaji wa Wilaya ya Temeke, anahamia Tanga kuwa naibu ofisa wa uhamiaji wa mkoa.
Pia, Julieth Sagamiko (Kitengo cha Hati za Kusafiria cha Makao Makuu) amehamishiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kuwa mfawidhi wa kituo na nafasi yake itashikwa na Fredrick Eustace Kiondo, huku Naibu Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Kagera, Hosea Kagimbo akihamishiwa Holili kuwa mfawidhi wa kituo.
Pia, alisema Kaimu Kamishna, Jenerali wa Uhamiaji, Victoria Lembeli amewabadilisha vituo vya kazi maofisa hao 14, huku baadhi ya maofisa wakistaafu utumishi wa umma akiwamo aliyekuwa mfawidhi wa kituo cha Holili, Kaimu Kamishna, Alphonce Tishe
0 comments:
Post a Comment