Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa taarifa ya ugonjwa wa Figo ambapo katika tafiti mbalimbali zimezofanywa inaonyesha kuwa ugonjwa huo upo na unaendelea kuongezeka nchini.
Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Figo mwaka 2016 ni “Chukua Hatua Mapema Kuepuka Magonjwa ya Figo kwa Watoto”. Kauli mbiu hii inalenga kuhamasisha jamii juu ya matatizo ya figo yanayoikabili jamii yetu hususani watoto.
Kwa watu wazima chanzo kikubwa cha magonjwa ya figo ni ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu, pia utumiaji wa dawa za mitishamba na magonjwa ya kuambukiza kama ilivyo kwa watoto yanaweza kuathiri figo kwa watu wazima, yapo pia magonjwa mengi ambayo huathiri figo moja kwa moja mfano mawe ya figo na njia ya mkojo.
Tafiti za ugonjwa wa figo zinaonyesha kuwa kati ya mwezi Agosti 2014 na Februari 2015 kati ya watoto 513 waliopimwa magonjwa ya figo katika Hospitali za Bugando na Sekou Toure asilimia 16.2% walikuwa na matatizo ya figo. Katika utafiti huo ilionekana watoto waliokuwa na magonjwa ya figo walikuwa na malaria, ugonjwa wa seli mundu (sickle cell anaemia) maambukizi ya bakteria kwenye koo na ngozi na kutumia mitishamba kabla ya kufika Hospitali. Utafiti huu unaonyesha wazi uwepo wa matatizo ya figo kwa watoto.
Utafiti mwingine uliofanyika Mkoani Kilimanjaro kati ya mwezi Januari na Juni 2014, uliohusisha watu 481 kutoka katika kaya 146, asilimia 7% walionekana kuwa na matatizo ya figo. Utafiti huu ulionyesha uhusiano wa karibu kati ya uwepo wa tatizo la figo na ugonjwa wa kisukari, shinikizo la damu na matumizi ya mitishamba.
Serikali inaendelea na utekelezaji wa Sera ya Afya (2007) ambayo inalenga kutoa huduma kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo matatizo ya figo. Aidha, Serikali, Sekta Binafsi, Mashirika ya Kimataifa na Taasisi zinazotoa huduma bila faida zinaendelea kuandaa na kurekebisha Sheria, Kanuni na Taratibu zinazoimarisha uzuiaji na udhibiti wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Hospitali zenye wataalamu wa magonjwa ya figo ni Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali ya KCMC, Hospitali ya Rufaa Mbeya, Hospitali ya Bugando na Hospitali ya Benjamin William Mkapa iliyopo Dodoma na mpaka sasa wagonjwa 190 wakiwemo watoto wawili wamepata huduma ya kupandikizwa figo na wanapata huduma katika kitengo cha figo Muhimbili na katika Hospitali nyingine za rufaa.
Pia Serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha huduma za upandikizaji wa figo zinapatikana hapa nchini haraka iwezekanavyo ili kupunguza gharama za kupelekwa wagonjwa nje ya nchi na kutoa huduma kwa watanzania wengi zaidi.
Aidha Wizara inatoa wito kwa kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa anapima afya yake na kwa wale ambao wameshajitambua kuwa na matatizo ya figo, kisukari na shinikizo la damu lakini hawatumii huduma za afya ipasavyo, wanaaswa kutumia huduma za afya zilizopo kwa manufaa ya afya zao na kuepusha athari zinazotokana na magonjwa hayo.
0 comments:
Post a Comment