Tuesday, 22 March 2016

Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi Toka Uganda Hadi Tanzania Uko Palepale soma ujue msimamo Dk Magufuli

 
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda mpaka Bandari ya Tanga utafanyika kama marais wa nchi hizo mbili walivyokubaliana.

Wameeleza kuwa kwa sasa makubaliano yako katika hatua za mwisho ili ujenzi wa mradi huo kuanza huku nchi za Kenya na Uganda wakiendelea na mazungumzo katika kufikia mwafaka wa jambo hilo.

Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dk James Mataragio alisema hivi karibuni kumekuwa na taarifa za mradi huo kukwama kutokana na Kenya kudaiwa kukubaliana na Uganda kupitisha mradi huo nchini mwao.

Akizungumzia suala hilo, Dk Mataragio alisema ni kweli awali kulikuwa na makubaliano ya nchi hizo mbili kupitisha mradi huo Kenya kutoka Hoima hadi Bandari ya Lamu, lakini kwa sababu mbalimbali Uganda waliamua kupitisha Bandari ya Tanga.

Alieleza ingawa umbali kutoka Uganda hadi bandari za Kenya ni karibu kwa kilometa chache kuliko Tanga zipo sababu zilizofanya bomba hilo kufikishwa Tanga. Sababu hizo ni pamoja na gharama kubwa za ujenzi kwenda Kenya na bandari ya Tanga kuwa na kingo za asili hivyo kuweza kusafirisha mafuta mwaka mzima.

Alisema pia ujenzi wa bomba hilo hadi bandari ya Tanga haupiti sehemu yenye makazi ya watu wengi hivyo kupunguza gharama, huku bomba likipita maeneo mengi ya tambarare bila kuwa na miinuko inayofanya kuongeza gharama za kupampu.

Alisema tayari timu za wataalamu zimekutana na kukubaliana masuala kadhaa ya ujenzi huo pamoja na kusaini mpango wa utekelezaji wa mradi. 

Dk Mataragio alisema kuhusu gharama ni kawaida siyo kubwa kama inavyoelezwa na baadhi ya watu hivyo ni vema watanzania wakaelewa kuwa hakuna tatizo la kukwama kwa mradi huo kwa sababu yoyote.

Kampuni zinazozalisha mafuta nchini Uganda ni Tullow kutoka Ireland, Kampuni ya Ufaransa ya Total na Kampuni ya CNOC kutoka China.

Wakati hayo yakielezwa hivi karibuni, Makamu wa Rais wa Kampuni ya Total Afrika Mashariki, Javier Rielo alimueleza Rais John Magufuli kuwa kampuni hiyo itaanza ujenzi huo haraka iwezekanavyo, kwa kuwa fedha za kutekeleza mradi huo zipo.

Bomba hilo la kutoka Tanga hadi Uganda litakuwa na urefu wa kilometa 1,410 na litasafirisha mafuta ghafi kutoka ziwa Albert nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga na litajengwa kwa gharama ya Dola za Marekani bilioni nne.

Unatarajiwa kuzalisha ajira za moja kwa moja 1,500 na ajira zisizo za moja kwa moja 20,000 huku ukitarajia kukamilika baada ya miaka mitatu hadi minne.

0 comments: