Tuesday, 15 March 2016

Profesa Baregu: Utawala wa Rais Magufuli Ni Wa Kijeshi


SIKU moja baada ya Rais Dk. John Magufuli kuteua wakuu wa mikoa wapya, mtaalamu wa sayansi ya siasa, Profesa Mwesiga Baregu, ameibuka na kusema kuwa kuwapo kwa wanajeshi wengi wastaafu katika uteuzi huo inadhihirisha wazi kuna dalili za utawala wa kijeshi nchini.
 
Profesa Baregu amesema kuwa  wanajeshi huwa hawana hulka ya kidemokrasia.

“Kitu kimoja kinachojitokeza kwenye uteuzi huu ni kuwepo kwa wanajeshi wastaafu, na mimi ninavyoelewa wanajeshi huwa hawana hulka za kidemokrasia. Hii inaonyesha wazi kwamba utawala huu ni wa kijeshi,” alisema.

Profesa Baregu ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alisema haileti picha nzuri kuwapo kwa wanajeshi wengi katika utawala kwa sababu tawala za mikoa na wilaya ni saula la kiraia na demokrasia zaidi.

Alisema rasimu ya katiba ambayo yeye alikuwa mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ilipendekeza kupitia upya tawala za mikoa na kupunguza idadi yake.

“Kutokana na hilo, mamlaka ya wananchi inamezwa kwa sababu wakuu wa mikoa na wilaya ni wengi na kunakuwepo na mgongano mkubwa,” alisema.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ali, alisema uteuzi wa wakuu wa mikoa na wilaya ni wa rais na wanaoteuliwa ni watu mchanganyiko.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ruaha (Ruco), Profesa Gaudence Mpangala, alisema kila anapoingia kiongozi mpya anaunda timu ambayo anaona ataendana nayo.

0 comments: