Serikali imesema haina mpango wa kubadili vyeti vya wanafunzi waliomaliza kidato cha sita mwaka jana kutoka kwenye mfumo wa alama za GPA kwenda Divisheni.
Msimamo huo wa serikali, umetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako.
Amesema serikali haina mpango wa kubadili mfumo huo wa vyeti kwani tangu awali wanafunzi walisoma kwa mfumo wa GPA na vyeti vilitoka kwa mfumo huo.
“Hatuwezi kubadili vyeti hivyo, isipokuwa vimehitajika kwa ajili ya marekebisho madogo ambayo Katibu Mkuu wa Wizara, aliyasema lakini siyo kubadili kwenda mfumo wa divisheni,” alisema.
Februari mwaka huu, Baraza la Taifa la Mitihani (Necta), lilitangaza kusitishwa kwa ugawaji wa vyeti vya kidato cha sita kwa wanafunzi waliohitimu mwaka 2015, huku likiagiza kuwa vile vilivyokwisha gawanywa kwa wahitimu hao vinatakiwa kurejeshwa kwenye chombo hicho.
Hata hivyo, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk, Charles Msonde, hakubainisha marekebisho ambayo wanatakiwa kuyafanya kwenye vyeti hivyo na badala yake kudai baraza linataka kujiridhisha na baadhi ya vitu.
Hatua hiyo ya kubadili vyeti hivyo iliibua utata mkubwa, huku baadhi ya wadau wakiwamo maofisa elimu, wakihisi Necta huenda inalenga kuvibadili vyeti hivyo kutoka kwenye mfumo wa wastani wa alama (GPA), kwenda kwenye ule wa jumla (division).
0 comments:
Post a Comment