Zikiwa zimebakia siku saba kufanyika marudio ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar, kumejitokeza viasharia vya uvunjifu wa amani kwa kuharibiwa majengo ya Serikali na nyumba za watu binafsi.
Usiku wa kuamkia jana, Kituo cha Afya cha Kiuyu Minungwini, Maskani ya CCM Junguni pamoja na nyumba za wananchi katika maeneo ya Kangagani, Makangale, Msuka, Tumbe na Shumba, zimeteketezwa kwa moto na watu wasiofahamika.
Akizungumza kwa nyakati tofauti alipotembelea waathirika, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud mohamed alilaani kitendo hicho.
Alisema kinachoonekana, hujuma hizo zinapangwa na watu wasioitakia mema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kwa lengo la kutaka kuwajengea hofu wananchi, nchi inapoelekea kwenye uchaguzi wa marudio, Machi 20.
Hata hivyo, aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali kupitia vyombo vya ulinzi na usalama, itachukua hatua za haraka ili kuwabaini wote waliohusika na hujuma hiyo.
“Hivi ni vitendo vya makusudi, haiwezekani matukio hayo yote yatokee siku moja katika maeneo tofauti na kwa wakati mmoja, tutahakikisha wahusika tunawasaka na kuwafikisha mahakamani,”alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Omar Khamis Othman ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuongeza doria ili kuhakikisha amani na utulivu unadumishwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Hassan Nassir Ali aliahidi kuwasaka na kuwachukulia hatua watakaobainika kuhusika kwa matukio hayo.
Alitoa rai kwa wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa za watu wanaowatilia shaka katika maeneo yao.
“Tusiwaonee haya hawa watu, wanachangia kurudisha nyuma maendeleo yenu, mkiwaficha mtakuwa mnajiumiza wenyewe,”alisema kamanda huyo.
0 comments:
Post a Comment