Thursday, 5 September 2013

MTALII ASHAMBULIWA NA KUUAWA NA TEMBO HIFADHI YA TAIFA YA TARANGIRE

Raia mmoja wa Marekani, Thomas Vardon Mcaffe mwenye umri wa miaka 58, ameuawa baada ya kushambuliwa na kundi la tembo wakati akifanya shughuli za utalii katika hifadhi ya Taifa Tarangire iliyoko mkoani Manyara

Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Manyara, Mussa Marambo, ameiambia TBC kuwa, tukio hilo limetokea juzi saa 2 asubuhi wakati mtalii huyo kutoka Jimbo la Califonia nchini Marekani akiwa na wenzake wawili walipokuwa wakitalii katika hifadhi hiyo.

Kamishna Msaidizi wa Polisi Marambo amebainisha kuwa watalii hao walikimbizwa na kundi la tembo wapatao 50 wenye hasira, ambapo katika jitihada za kujihami, marehemu Thomas alikwama kwenye tope na kushambuliwa kwa kukanyagwa na tembo hao huku wenzake wawili wakifanikiwa kujiokoa.

Jitihada za kuokoa uhai wa marehemu baada ya kukimbizwa katika zahanati ya Tarangire ziligonga mwamba kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata wakati wa tukio hilo.

Mwili wa Merehemu umesafirishwa kwa ndege na kuhifadhiwa katika hospitali ya Selian, Arusha kwa uchunguzi zaidi wakati taratibu za kuukabidhi mwili wake kwa  ubalozi wa Marekani hapa nchini kwa ajili ya kuurejesha kwao inafanywa.

Benny Mwaipaja, 
TBC - Manyara.

0 comments: