Dodoma.Wabunge wa Kambi ya Upinzani Bungeni jana
jioni walitoka ndani ya Ukumbi wa Bunge, baada ya kupuuzwa kwa mwongozo
wao wa kutaka kuahirishwa kujadiliwa kwa Muswada wa Marekebisho ya
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, hadi hapo Zanzibar itakaposhirikishwa.
Wabunge waliotoka bungeni jana yapata saa 12.15 ni kutoka vyama vya Chadema, CUF na NCCR- Mageuzi huku Mbunge wa Vunjo na Mwenyekiti wa Taifa wa Tanzania Labour Party (TLP, Augustine Mrema akiendelea kubaki ukumbini.
Kitendo cha wabunge hao wa upinzani kilionekana kuwakera baadhi ya wabunge wa CCM, ambao walisikika wakiwakejeli kwa kupiga meza huku wakisema: “Kwendeni zenu, tumewazoea.”
Wakati wabunge hao wakiondoka, Naibu Spika wa
Bunge, Job Ndugai, alikuwa akiwasisitiza wabunge wanaobakia wawe
watulivu, maana kuna usalama wa kutosha ndani ya ukumbi huo.
“Mnaotoka nimewaona wote na mnanijua,” alisikika Naibu Spika Ndugai akiwatahadharisha wabunge wa upinzani waliosusa mjadala huo.
Wabunge wa CCM waliendeleza vituko ambapo baada ya wapinzani kutoka, wabunge Juma Nkamia (Kondoa Kusini), Hilary Aeshi ( Sumbawanga Mjini) na Murtaza Mangungu (Kilwa Kaskazini) walikwenda kukaa katika viti vya kambi ya upinzani.
Kabla ya kutoka kwa wabunge hao wabunge wawili kutoka CUF waliomba mwongozo wa Spika, wakitaka muswada huo kuondolewa ili kuwapa nafasi Wanzanzibar kutoa maoni yao.
Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mohamed Mnyaa (CUF)
aliomba mwongozo akitaka muswada huo uondolewe, hadi hapo Wazanzibar
watakaposikilizwa.
Alisema kuwa kwa maoni ya Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala wamesikiliza maoni ya wadau wengi, lakini Zanzibar hawakwenda kuwasikiliza wadau wa eneo hilo.
“Na hili suala zima katika masuala ya katiba linahitaji usawa wa washirika, tunazungumza kitu kinachohusiana na Zanzibar na Tanzania Bara, ili kupata maoni ya nchi nzima kuna uhalali gani wa Bunge hili kuendelea na mjadala huu?” alihoji.
Hata hivyo, alikatizwa na kelele za Mbunge wa Viti Maalumu, Pindi Chana (CCM), ambaye alitoa taarifa kuwa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ilialika wajumbe mbalimbali ikiwamo Zanzibar.
“Miongoni wa wajumbe walioalikwa ni pamoja na
Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Zanzibar pamoja na wadau
mbalimbali ambao walikuja mbele ya Katiba,” alisema Pindi ambaye pia ni
Mwenyekiti wa kamati hiyo.
Na Waandishi Wetu
Mwananchi
Posted Jumatano,Septemba4 2013
Posted Jumatano,Septemba4 2013
0 comments:
Post a Comment