Jeshi la Polisi limeendelea na kamatakamata ya wapinzani wa vyama vinavyounda Ukawa katika maeneo mbalimbali likieleza sababu tofauti za kijinai zinazohusishwa na masuala ya kisiasa.
Mpaka sasa wabunge wa upinzani waliokamatwa ni; Halima Mdee (Kawe), Mwita Waitara (Ukonga) na Peter Lijualikali (Kilombero), wote wa Chadema na baadhi ya madiwani wa chama hicho katika Jiji la Dar es Salaam.
Vilevile, imeelezwa kuwa Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea alikuwa anatafutwa kuunguanishwa na wenzake.
Pia, baadhi ya wanasiasa wa CUF Zanzibar wamekamatwa na kuhojiwa kwa madai ya kuwatusi viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Viongozi wa CUF waliohojiwa na polisi mpaka sasa ni Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi, Omar Ali Shehe na Kiongozi wa Mkakati wa Ushindi, Mohamed Sultan Mugheir ‘Eddy Riyami’ ambaye yuko nje kwa dhamana.
Mbali na viongozi hao, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui jana amepatiwa barua ya wito na Polisi Zanzibar ikielezwa kuna mambo yanamhusu.
Hii ni mara ya pili kwa Mazrui kuitwa polisi tangu kufutwa kwa uchaguzi wa Oktoba 25, huku CUF ikidai kuwa huo ni mwendelezo wa mkakati maalumu dhidi ya viongozi wa chama hicho.
Jana, Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa Umma wa CUF, Maalim Hamad Masoud Hamad alidai kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya kisiasa ya kutaka kumkamata kila kiongozi wa juu wa CUF kuelekea uchaguzi wa marudio.
“Kwa viongozi wa CUF hili halishangazi, nahisi ingelikuwa ni hatua ya kushangaza sana iwapo wanaoitwa kuhojiwa na polisi ni viongozi wa vyama vingine.
"Sisi upande wetu hili ni jambo la kawaida mno na watu wasishangae,”alisema.
Mazrui ambaye pia alikuwa Waziri wa Biashara na Uwekezaji, ametakiwa kuripoti Makao Makuu ya Polisi, Ofisi ya Upelelezi Ziwani mjini hapa kesho saa 2.00 asubuhi na kuonana na mkurugenzi wa makosa ya jinai Zanzibar.
Polisi Zanzibar imethibitisha kuwapo wito huo ikisema kuna mambo muhimu yanayomhusu mwanasiasa huyo.
0 comments:
Post a Comment