WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa(Pichani) amesema watumishi wa umma wako huru kuhamia kokote wapendako lakini wahakikishe wanaenda huko wakiwa safi na kamwe mtu asiharibu kazi kazi akitarajia kuwa atahamishiwa sehemu nyingine.
"Serikali hii haina utumishi kwa mtu aliyeharibu kazi,usije ukaharibu hapa Itilima ukadhani utaenda Bunda kuendelea na kazi. Serikali ya awamu hii haina nafasi na watumishi wa aina hiyo," amesema.
Waziri Mkuu ametoa onyo hilo leo (Ijumaa, Machi 4, 2016) wakati akizungumza na watumishi wa wilaya ya Itilima kwenye ukumbi wa Halmashauri ya wilaya hiyo ambao ameuzindua leo hii wilayani Itilima, mkoani Simiyu.
"Watumishi wenzangu huu ni wakati wa kubadilika na kuona mwelekeo wa Serikali hii ya awamu ya tano ukoje. Jukumu letu ni kuwatumikia Watanzania wote bila kujali itikadi zao, rangi wala dini zao," alisisitiza.
Waziri Mkuu aliwahakikishia watumishi hao kwamba Serikali inatambua changamoto walizonazo kutokana na upya wa wilaya hiyo na mkoa huo na akawaahidi kuwa itaboresha mazingira yenu.
"Msiwaadhibu wananchi kwa kisingizio cha mazingira magumu ya kazi zenu, tunajua mnayo madai ya nauli, posho za mafunzo, kupandishwa madaraja na malimbikizo ya likizo," alisema huku akishangiliwa.
Alisema Serikali itayalipa madeni hayo japo haitamaliza yote kwa wakati mmoja ila ana uhakika wa kukamilisha walau kwa asilimia 80.
Mapema, akitoa taarifa ya wilaya hiyo, Mkuu wa wilaya hiyo, Bibi Georgina Bundala alisema wilaya hiyo iliyoanzishwa Machi 2012 na kupata Halmashauri Julai 2013 haina kituo cha polisi cha wilaya, haina gereza, Ofisi za TAKUKURU, mahakama ya wilaya wala benki.
Alisema wilaya hiyo haina hospitali ya wilaya ila akabainisha kuwa wamekwishatenga eneo la ekari 30 kwa ajili ya ujenzi huo.
"Pia tumekwishapima viwanja 123 na eneo la kujenga taasisi lenye ekari 143.8 limefanyiwa uthamini na fidia kukamilika," alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, MACHI 4, 2016.
0 comments:
Post a Comment