MKUU wa Majeshi Tanzania, Jenerali Davis Mwamunyange amewaongoza wanajeshi mbalimbali kuwaaga Majenerali 16 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ambao wamemaliza muda wa utumishi wao.
Sherehe hizo zilifanyika Uwanja wa Kambi ya Jeshi wa Twalipo, Mgulani jijini Dar es Salaam kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 6:30 mchana. Sherehe hizo ziliongozwa na bendi ya jeshi na gwaride maalumu.
Miongoni mwa waliomaliza muda wao ni Meja Jenerali Samuel Ndomba ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na hadi anastaafu alikuwa Mnadhimu Mkuu wa JWTZ.
Wengine ni Luteni Jenerali Paul Mella ambaye alikuwa Kamanda wa Majeshi ya Kulinda Amani ya Darfur, Sudan na Brigedia Jenerali Harold Mziray ambaye alikuwa Mkuu wa Shule ya Infantria, Arusha.
Majenerali wengine walioagwa ni Brigedia Jenerali Martin Mwankanye aliyekuwa Mkurugenzi wa Mahusiano ya Kimataifa jeshini, Brigedia Jenerali John Chacha aliyekuwa Kamanda wa Brigedi ya Tembo na Brigedia Jenerali Ezra Ngingwango aliyekuwa Mkuu wa Kikosi cha Ndege na Usafirishaji jeshini.
Brigedia Jenerali Mrisho Abdallah aliyekuwa Mratibu Miradi ya Maendeleo jeshini naye ameagwa kama ilivyo kwa Brigedia Jenerali Emmanuel Maganga aliyekuwa Mkuu, Tawi la Ukaguzi jeshini, Brigedia Augustino Gailanga aliyekuwa Mkuu wa Tawi Jeshi la Akiba, Brigedia Jenerali Luhindi Msangi aliyekuwa Mkuu wa Chuo cha Sayansi za Tiba Lugalo, Dar es Salaam na Meja Jenerali Raphael Muhuga wa JKT.
Wengine ni Meja Jenerali Charles Muzanila aliyekuwa Mkuu wa Shirika la Mzinga Morogoro, Meja Jenerali Ezekiel Kyunga aliyekuwa Mkuu wa Chuo cha Ukamanda na Unadhimu kilichopo Duluti mkoani Arusha, Meja Jenerali Joseph Kapwani aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Anga, Meja Jenerali Vincent Mritaba aliyekuwa Mkuu wa Utumishi jeshini na Meja Jenerali Salum Kijuu, Mkuu wa Jeshi la Nchi Kavu.
Brigedia Jenerali mstaafu, Msangi (kulia mbele), akikagua gwaride maalumu waliloandaliwa maofisa hao wastafu wakati wakiagwa rasmi baada ya kumaliza utumishi wao jeshini.
Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), mstaafu Meja Jenerali, Raphael Muhuga, akikagua gwaride hilo.
Mkuu wa Majeshi, Jenerali, Davis Mwamunyange (kushoto), akisalimiana na kumpongeza Mkuu wa Vikosi vya Kulinda Amani Umoja wa Mataifa, Luteni Jenerali mstaafu, Paul Ignas Meela katika hafla hiyo.
0 comments:
Post a Comment