Maofisa wawili wa benchi la Ufundi la timu ya taifa ya Misri wanatarajiwa kuwasili nchini wakati wowote kwa ajili ya kuja kuandaa mazingira ya Mafarao watakapokuja Tanzania Juni kucheza mechi ya kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika.
Wawili hao, mtahmini michezo na mmoja wa makocha Wasaidizi, Mahmoud Fayez pamoja na Mkurugenzi wa Ufundi, Ehab Leheta.
Misri wanahitaji sare tu na Tanzania Juni 4, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ili kujihakikishia usukani wa Kundi G hivyo kufuzu AFCON ya mwakani Gabon.
Misri inaongoza Kundi G kwa pointi zake saba na itacheza mechi yake ya mwisho Dar es Salaam Juni 4.
Tanzania inashika mkia kwa pointi yake moja, ikifuatiwa na Nigeria yenye pointi mbili, lakini ina mechi mbili ambazo ikishinda zote itafikisha pointi saba na kulingana na Misri, hivyo timu ya kufuzu AFCON kuamuliwa kwa idadi ya mabao.
Na baada ya kujiridhisha kwamba kiwango cha soka ya Tanzania kimepanda, Misri imeupa uzito mkubwa mchezo huo kuhakikisha inafuata tiketi ya AFCON Dar es Salaam.
Tayari Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lina taarifa za ujio wa mabosi hao wa Mafarao na kwa upande wao, wanatarajiwa kukutana na kocha Mkuu, Charles Boniface Mkwasa kupanga programu ya maandalizi ya mchezo huo.
TFF inataka kuhakikisha Ligi Kuu inamalizika kwa wakati Mei ili upatikane muda wa kuipeleka Taifa Stars kambini nje ya nchi.
0 comments:
Post a Comment