Wednesday, 13 April 2016

Dereva TAXI Atiwa Mbaroni akituhumiwa Kubaka abiria


DEREVA teksi katika Manispaa ya Iringa, Elain Mahenge (27), anashikiliwa na polisi mkoani hapa kwa tuhuma za kumbaka mteja wake.

Mahenge, Mkazi wa Semtema, Kihesa katika Manispaa ya Iringa, anadaiwa alikutwa akifanya kitendo hicho dhidi ya mteja wake  saa 3:45 usiku.

Kitendo hicho cha ubakaji kimetokea ikiwa imepita takriban miezi miwili, tangu Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Iringa, kutoa elimu kwa wananchi wa Kihesa juu ya kuwafichua watu wanaodaiwa kufanya vitendo vya ubakaji.

Elimu hiyo ilitolewa kutokana na kuripotiwa kukithiri kwa vitendo hivyo, ikiwamo dhidi ya watoto wa kike na kuwalawiti watoto wa kiume, huku zaidi ya watu 10 wakiwa wameshakamatwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kujihusisha na unyama huo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Peter Kakamba, alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea Jumapili iliyopita, katika eneo la Kihesa. Alisema mtuhumiwa alikutwa akimbaka mteja wake huyo, ambaye ni mkazi wa Mgololo, Mufindi mkoani Iringa.

Kakamba alisema mteja huyo alimkodi dereva huyo, baada ya kushuka kwenye gari katika kituo kikuu cha mabasi cha Iringa na kumtaka ampeleke kwenye nyumba ya kulala wageni iliyoko Kihesa.

“Inadaiwa dereva teksi huyo alimchukua stendi hapo na kwenda alikoambiwa ampeleke lakini alipofika njiani kwenye giza alisimama na kisha kumbaka binti huyo,” alisema.

Kamanda Kakamba alisema wakati dereva huyo akiendelea kufanya kitendo hicho, binti huyo alipiga kelele ambazo zilisikika na askari polisi ambao waliokuwa doria usiku huo na wakati polisi wanafika eneo la tukio tayari mtuhumiwa alikuwa ameshamaliza kufanya kitendo hicho na ndipo walipomkamata.

Alisema kuwa mtuhumiwa yuko polisi na ushahidi umeonekana pale pale kwa kuwa mazingira na hali waliyokutwa nayo dereva na binti huyo, yalidhihirisha mtuhumiwa alitenda jambo hilo bila ya huruma tena kwa mteja wake, hivyo mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakani wakati wowote kuanzia sasa.

Aidha kamanda huyo aliwataka wakazi wa mji wa Iringa na viunga vyake kupanda teksi ambazo zimesajiliwa na si kupanda teksi bubu kama aliyokuwa ameipanda msichana aliyefanyikwa unyama huo.

0 comments: