MGANGA wa tiba za asili, Juma Ramadhani pamoja na mwanafunzi wa Chuo cha Utalii Masai, Saumu Mohamed (19) wanashikiliwa na Polisi mkoani Tanga kwa tuhuma za kuharibu mimba ya miezi saba.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Mihayo Msikhela aliwaambia waandishi wa habari jana, watuhumiwa hao ambao ni wakazi wa mtaa wa Sahare, walikamatwa Februari 29 mwaka huu saa 2:00 usiku katika mtaa huo ulio kata ya Mzingani.
Alisema kukamatwa kwao kumekuja baada ya wananchi kuokota maiti ya mtoto mchanga mwenye jinsia ya kike ambaye inadaiwa alikuwa ni mimba ya miezi saba.
“Siku hiyo ya tukio katika maeneo ya Sahare jijini Tanga aliokotwa mtoto wa kike ambaye ni mimba ya miezi saba. Inadaiwa mimba hiyo iliharibiwa na Saumu ambaye in mwanafunzi wa Chuo cha Utalii Masai cha mkoani hapa”.
Alisema na kuongeza: “Binti huyo kulingana na uchunguzi wetu wa awali anadaiwa kunywa dawa ya kutoa mimba kwa kutumia dawa maalumu ambayo alipewa na mganga wa kienyeji aitwaye Juma Ramadhani na ndipo ikaharibu ujauzito huo na kisha Saumu alipofanikiwa kujifungua, akaamua kutupa maiti ya mtoto huyo ambayo baadaye iliokotwa na wananchi.”
Alisema watuhumiwa wote wanashikiliwa na Polisi na watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika
0 comments:
Post a Comment